Habari za michezo

Barcelona Ilimuonea Hapa Hapa Mtanzania

Vardo June 29, 2026 9:55 am

KUNA baadhi ya watu bado wanajiuliza, ilikuwaje hadi kijana Mtanzania, Barka Seif, akajikuta akisajiliwa na akademi maarufu ya Barcelona, La Masia.

Jibu ni rahisi. Barka alitumia vyema nafasi aliyopata alipokutana na vijana wa Barcelona katika mchezo wa ligi akiwa anakipiga katika kikosi cha CF Damm, moja ya akademi zinazofanya vizuri katika eneo la Catalonia.

Safari ya kinda huyo inavutia. Mwaka mmoja uliopita alicheza dhidi ya Barcelona akiwa na kikosi cha vijana cha CF Damm, akitafuta kuonyesha uwezo wake kama ilivyo kwa vijana wengi wenye ndoto ya siku moja kucheza katika klabu kubwa duniani. Hakujua kwamba mchezo huo ungekuwa mwanzo wa kubadili maisha yake.

Kilichovutia zaidi ni kiwango alichokionyesha katika mchezo huo, ambapo aliifunga Barcelona mabao matatu (hat-trick), jambo lililowafanya wasaka vipaji wa klabu hiyo kuanza kumfuatilia kwa karibu.

Akiwa na CF Damm, Barka aliendelea kuthibitisha uwezo wake kwa kucheza mechi 28 za ligi ya vijana na kufunga mabao 41, rekodi iliyomfanya amalize kinara wa ufungaji.

Mbali na mabao hayo, alionyesha kiwango kilichomfanya achaguliwe katika kikosi bora cha vijana chini ya miaka 12 cha Shirikisho la Soka la Catalonia, hatua iliyomfanya kuwa mmoja wa Watanzania wachache kufikia kiwango hicho katika mfumo wa soka wa Hispania.

Baada ya kipindi cha ufuatiliaji, Barcelona ilifanya uamuzi wa kumpa nafasi ya kujiunga na akademi maarufu ya La Masia, iliyozalisha mastaa wengi waliotawala soka la dunia.

Akizungumzia mafanikio hayo, baba mzazi wa Barka, Seif Mpanda, amesema kwa sasa jambo kubwa ni kumuombea mwanawe apate nafasi ya kucheza na kuonyesha kipaji chake.

“Kikubwa sasa hivi ni kumuombea kijana apate nafasi ya kucheza na aonyeshe kipaji chake, hilo ndilo muhimu kwa sasa,” amesema Seif Mpanda.

Kikwazo Kimoja Chazuia Mwalimu Kusaini Simba Mkenya Presha Yaanza Mtibwa Sugar