Simba SC

Kikwazo Kimoja Chazuia Mwalimu Kusaini Simba

Vardo June 29, 2026 9:50 am

UONGOZI wa Simba SC umeweka wazi dhamira ya kuendelea kuwa na mshambuliaji Selemani Mwalimu katika kikosi cha msimu wa 2026/27, baada ya nyota huyo kuonyesha kiwango cha kuvutia tangu alipojiunga na Wekundu wa Msimbazi kwa mkopo.

Hata hivyo, ndoto ya Simba ya kumbakisha Mwalimu itategemea mafanikio ya mazungumzo yatakayofanyika kati ya klabu hiyo na Wydad AC ya Morocco, ambayo inamiliki haki za mchezaji huyo.

 

Taarifa zinaeleza kuwa Kocha Mkuu Steve Barker amemjumuisha Mwalimu kwenye orodha ya wachezaji anaotaka waendelee kuwa sehemu ya kikosi chake msimu ujao, akivutiwa na mchango wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji.

Chanzo cha habari kimebainisha kuwa mkataba wa sasa wa mkopo wa Mwalimu hauna kipengele cha kuongeza muda wa mkopo wala kumpa Simba nafasi ya kumnunua moja kwa moja.

 

Baada ya mkataba huo kumalizika, mshambuliaji huyo atalazimika kurejea Wydad AC isipokuwa pande hizo mbili zifikie makubaliano mapya.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa Wydad AC haina pingamizi la kumuachia mchezaji huyo kwa uhamisho wa moja kwa moja, jambo linaloipa Simba matumaini ya kufanikisha dili hilo ikiwa itakubaliana na masharti ya kifedha yatakayowekwa.

Ada ya usajili ndiyo inaelezwa kuwa kikwazo kikubwa kinachoweza kuamua hatma ya mazungumzo hayo, huku Simba ikihitajika kufikia mwafaka wa kifedha na Wydad ili kukamilisha usajili huo.

Kwa upande wa mchezaji, taarifa zinaeleza kuwa Mwalimu ameipa Simba kipaumbele licha ya kuvutiwa na klabu nyingine. Inaelezwa kuwa yuko tayari kusubiri uamuzi wa Wekundu wa Msimbazi kabla ya kuanza kusikiliza ofa nyingine.

 

Mustakabali wake utaamuliwa na matokeo ya mazungumzo kati ya Simba na Wydad AC, ambayo yakifanikiwa, yatawawezesha mashabiki wa Msimbazi kuendelea kumuona mshambuliaji huyo akivaa jezi nyekundu na nyeupe msimu ujao.

Yanga Wamuwinda Kocha Simba, Ushindani Wa Al Hilal Wapamba Moto Barcelona Ilimuonea Hapa Hapa Mtanzania