Yanga Wamuwinda Kocha Simba, Ushindani Wa Al Hilal Wapamba Moto
KATIKA Harakati za Yanga kusaka kocha mkuu mpya zimeingia katika hatua mpya baada ya klabu hiyo kuanza mazungumzo na kocha raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids, aliyewahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Simba SC.
Uongozi wa mabingwa hao wa Tanzania Bara unatajwa kumuweka Fadlu kwenye orodha ya makocha wanaopewa kipaumbele kuelekea maandalizi ya msimu mpya.
Fadlu, ambaye pia aliwahi kuifundisha Raja Club Athletic ya Morocco, amejijengea heshima kubwa katika soka la Afrika kutokana na uzoefu wake wa kufundisha katika ligi mbalimbali zenye ushindani mkubwa.
Sifa hizo zimemfanya kuwa mmoja wa makocha wanaovutia viongozi wa Yanga katika mchakato wa kutafuta mrithi wa benchi la ufundi.
Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa Rais wa Yanga, Hersi Said, tayari amefanya mawasiliano na wakala wa kocha huyo na kuwasilisha nia ya klabu hiyo ya kutaka kumsajili.
Hata hivyo, uamuzi wa mwisho bado haujafikiwa huku pande zote zikiendelea na mazungumzo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Fadlu anatarajiwa kusafiri kwenda Cape Town, Afrika Kusini, wiki hii kwa ajili ya kukutana na wakala wake.
Chanzo cha habari kimesema Mkutano huo unatarajiwa kujadili mustakabali wake pamoja na ofa mbalimbali ambazo tayari zimewasilishwa kwake kutoka ndani na nje ya Afrika.
“Yanga si klabu pekee inayowania huduma za kocha huyo, Mabingwa wa Sudan, Al Hilal, nao wameonyesha nia ya kumsajili Fadlu, kuwa mazungumzo ya awali kati ya pande hizo tayari yameanza.
Ushindani huo unaifanya hatma ya Fadlu kubaki mikononi mwake, kwani anatarajiwa kupitia kwa makini kila ofa atakayopokea kabla ya kufanya uamuzi wa klabu atakayoihudumia katika msimu ujao,” kimesema.