Habari za michezo

Argentina Yazindua Sanamu La Messi

Vardo June 29, 2026 7:32 pm

NEUQUEN, ARGENTINA: ARGENTINA imezindua sanamu ya Messi yenye uzito wa tani 70, ikiwa ni kubwa zaidi duniani ambayo inalenga kuvutia watalii katika Jiji la Cutral Co lililopo mkoani Neuquen ambalo linaaminika kuwa ndilo kubwa zaidi duniani kuwahi kujengwa kwa heshima ya nyota huyo wa soka.

Taarifa zinaeleza kwamba sanamu hiklo lenye ukubwa urefu wa mita 26 la nahodha huyo wa timu ya taifa limewekwa kando ya Barabara Kuu ya Taifa Namba 22 na Manuel Savio, ikiwa alama mpya ya mji huo kwenye mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafiri nchini.

Sanamu hilo limebuniwa na msanii wa eneo hilo, Aldo Beroisa, likimuonyesha Messi akiwa amevaa jezi ya timu ya taifa ya Argentina huku akiwa ameshika Kombe la Dunia walilolinyakua nchini Qatar 2022.

Muundo huo umejengwa kwa fremu ya chuma na kufunikwa kwa kiasi kikubwa na saruji, ukiwa na uzito unaokadiriwa kufikia tani 70. Kwa ukubwa huo, umeweka rekodi mpya kama sanamu kubwa zaidi kuwahi kujengwa kwa heshima ya mshindi huyo wa Ballon d’Or.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi, viongozi wa jiji hilo wamesema sanamu hilo ni ishara ya kumuenzi Messi na pia alama ya fahari ya taifa baada ya ushindi wa Argentina wa Kombe la Dunia 2022. Sherehe za uzinduzi zilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu, watalii na mashabiki wa soka waliovalia jezi za Argentina na kupeperusha bendera za taifa hilo.

Mamlaka za Cutral Co zinaamini kuwa sanamu hilo litachochea utalii katika Mkoa wa Neuquen kwa kuvutia mashabiki wa Messi na soka la Argentina kutoka sehemu mbalimbali duniani, huku likiongeza hadhi ya mji huo ambao tayari unafahamika kama “mji mkuu wa sanamu”.

Kabla ya hapo, rekodi ya sanamu refu zaidi ya Messi ilikuwa ikishikiliwa na lile la mita 21 lililojengwa Kolkata, India. Hata hivyo, lilibomolewa baada ya wananchi kuripoti kuwa lilikuwa likiyumba kutokana na upepo.

Uzinduzi wa sanamu la Messi umefanyika wakati akiendelea kuiongoza Argentina katika Kombe la Dunia 2026, ambako nyota huyo mwenye umri wa miaka 39 alianza kwa kiwango cha juu akifunga hat-trick katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Algeria kabla ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Austria. Kwa mabao hayo, Messi ameweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji bora wa muda wote.

Nyota Barca Aichomolea Man United Burudika Na Non-Stop Win & Go Bila Dau La Ziada