Home Habari za michezo PEDRO AWEKA WAZI HATUA YA MWISHO KWA MZIZE

PEDRO AWEKA WAZI HATUA YA MWISHO KWA MZIZE

0

LICHA ya mshambuliaji wa Yanga , Clement Mzize, kuonyesha maendeleo mazuri katika mchakato wake wa kupona, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pedro Goncalves, amesema nyota huyo bado hajawa tayari kwa asilimia 100 kucheza dakika 90 mfululizo.

Pedro amefafanua kuwa Mzize tayari ameanza mazoezi mepesi na amepewa dakika chache katika baadhi ya michezo ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB kwa lengo la kupima utayari wake. Hata hivyo, bado hajafikia kiwango cha utimamu wa mwili kinachohitajika kuhimili presha na kasi ya mchezo mzima.

Kocha huyo amesema kumekuwa na maswali mengi kutoka kwa mashabiki kuhusu sababu ya mshambuliaji huyo kutotumika mara kwa mara, lakini akasisitiza kuwa benchi la ufundi linafuata utaratibu wa kitabibu ili kuhakikisha mchezaji anarejea akiwa fiti kabisa.

“Mzize alianza kurejea uwanjani kwa kupewa dakika chache ili kupima hali yake, lakini bado hajafikia kiwango kinachoturidhisha kumpa jukumu la kucheza dakika zote 90. Tunahitaji kuhakikisha anakuwa fiti kwa asilimia mia moja kabla ya kumpa mzigo mkubwa wa mechi nzima,” amesema Pedro.

Ameongeza kuwa majibu ya vipimo vya mwisho yanatarajiwa kupatikana ndani ya siku mbili au tatu zijazo, ambayo yataamua rasmi ni lini mchezaji huyo ataungana kikamilifu na kikosi katika harakati za kuipambania timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali.

Pedro amesisitiza kuwa hawako tayari kuhatarisha afya ya mchezaji kwa kumrejesha mapema, huku akiwaomba mashabiki kuwa na subira katika kipindi hiki cha mpito wakati timu ikiendelea na majukumu yake ya ushindani.