Gamondiatoa Tamko Kali: Hatujasafiri Kwenda Nigeria Kuwa Ngazi ya Mtu!
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Miguel Gamondi, ameweka wazi msimamo wake kuelekea mchezo wa kufuzu fainali za AFCON 2027 dhidi ya Nigeria, akisisitiza kuwa kikosi chake kimeenda kupigania ushindi na si kuwa daraja la wapinzani wao.
Taifa Stars na Super Eagles zinatarajiwa kushuka dimbani kesho Ijumaa, Novemba 13, 2026, kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio, jijini Uyo, huku mchezo wa marudiano ukipangwa kufanyika Jumanne, Novemba 17, kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Akizungumza kutoka Nigeria, Gamondi alikiri ubora na historia ya Nigeria lakini akasisitiza kuwa hawatatoroka jukumu la kupigania matokeo mazuri.
“Tunaijua Nigeria, tunaiheshimu na tunajua historia yake. Lakini tutaikabili kama tunatafuta nafasi ya kufuzu. Kamwe hatutaki kuwa daraja wala ngazi ya Nigeria kufikia malengo yake,” alisema Gamondi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Timu za Taifa wa TFF, Almasi Kasongo, naye alisisitiza kuwa timu haina hofu na iko tayari kwa pambano hilo la dakika 90.
Wakati Nigeria ikimkosa mshambuliaji wake staa Victor Osimhen anayesumbuliwa na jeraha, Taifa Stars nayo imefanya mabadiliko madogo baada ya kocha kumuondoa Clement Mzize na Dickson Job kupumzishwa, huku akimuongeza winga wa Azam FC, Iddy Nado, kikosini.