Hamis Kigwangalla Simba SC
Simba SC

Kigwangalla Afunguka Uenyekiti Simba SC: “Ndoto Yangu Ni Kununua Hisa”

Vardo November 12, 2026 12:37 pm

Aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla, ameweka wazi msimamo wake kuhusu habari zinazomhusisha na kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Klabu ya Simba SC katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Januari 30, 2026.

Kigwangalla ameeleza kuwa hana mpango wala nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya klabu hiyo kwa sasa, bali ndoto na lengo lake kubwa ni kuwekeza kwa kununua hisa za Simba Sports Club pindi fursa itakapopatikana.

Kauli hiyo ya Dk. Kigwangalla imekuja kufuatia kuwepo kwa majadiliano yaliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, ambapo wanachama na mashabiki wengi wa Simba wamekuwa wakitaja jina lake kama miongoni mwa watu wanaofaa kuchukua mikoba ya uongozi wa klabu hiyo.

“Sina Mpango wa Kugombea” – Kigwangalla

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dk. Kigwangalla amewashukuru wote waliomwamini lakini akasisitiza kuwa mwelekeo wake kwa sasa uko tofauti kabisa.

“Watu wengi wamekuwa wakinitafuta na kunihamasisha nichukue uongozi wa Simba Sports Club. Naona hata media zimeanza kuniandika, huku kukiwa na baadhi ya comments za kejeli. Kwanza, narudia kuwashukuru sana kwa imani hiyo. Lakini nirudie nilichokwisha kusema: Sina mpango wa kugombea nafasi yoyote ya uongozi Simba wala popote pale kwa sasa.”

“Kwa upande wa Simba, ningependa zaidi kuwa mwekezaji kwa kununua hisa za klabu,” aliongeza Dk. Kigwangalla.

Muda wa Kujitafakari na Kujenga Urithi wa Familia

Kigwangalla amefunguka zaidi kuhusu sababu za kujitenga na nafasi za uongozi wa umma na taasisi mbalimbali kwa sasa, akieleza kuwa amejipa muda wa kujitafakari na kuwekeza nguvu zake kwenye mambo binafsi na urithi wa familia yake.

Amesema hata baada ya kutokea fursa za kuwania Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) pamoja na nafasi za uongozi wa chama mkoani Tabora ambapo alihamasishwa sana na viongozi wenzake, aliamua kuzikataa kwa heshima.

“Bado natafakari sana kuhusu maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine dhidi ya kutumia muda na nguvu kujenga urithi kwa ajili ya familia yangu, hasa wajukuu zangu. Kuna watu wanaamini kwamba kushika nafasi ya uongozi wa umma, chama au taasisi ni fursa ya kujitengenezea fedha. Pengine kwa baadhi ni hivyo, lakini kwa wengi ukweli ni tofauti. Ni kujitoa na kutumia muda kujenga cha wote, wakati mwingine kwa gharama ya kuchelewesha kujenga cha kwako na cha familia yako,” alieleza.

Uchaguzi Mkuu wa Simba SC 2026

Katika Uchaguzi Mkuu wa Simba SC unaotarajiwa kufanyika Januari 30, 2026, wanachama wanatarajiwa kupiga kura kujaza nafasi moja (1) ya Uenyekiti wa Klabu pamoja na nafasi tano (5) za Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara: Mchakato, Vigezo na Siri Zake Wembley Hapatoshi! England Na Croatia Kukutana Tena