KUELEKEA mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya TRA United, Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema kikosi chake kinaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda huku akisisitiza kuwa lengo lao kubwa ni kuendelea kukusanya ushindi katika michezo ya ligi.
Barker ameyasema hayo akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kabla ya kuvaana na TRA United, akieleza kuwa wachezaji wake wako tayari kupambana kwa nguvu ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo muhimu.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani kuwakabili wenyeji wao TRA United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, katika pambano la kusaka alama tatu muhimu zitakazowasaidia kujiimarisha zaidi kwenye msimamo wa ligi.
Kocha huyo ameongeza kuwa maendeleo ya kikosi chake yanaonekana wazi kutokana na namna wachezaji wanavyozidi kuelewana uwanjani na kuonyesha kiwango kizuri katika michezo yao ya hivi karibuni.
Aidha, Barker amesema jambo linalompa faraja zaidi ni kwamba kikosi chake kwa sasa hakina majeruhi, hali inayompa nafasi pana ya kupanga kikosi bora kitakachoshuka dimbani kupambana na wapinzani wao.
“Tumefanya maandalizi mazuri na wachezaji wengi wako tayari kwa ajili ya kusaka alama muhimu katika mchezo huu. Haitakuwa rahisi kwa sababu kila timu inapambana kutafuta pointi muhimu,” amesema Barker.
Kocha huyo pia amewataka wachezaji wake kuendelea kudumisha nidhamu ya mchezo, kujituma na kupambana kwa nguvu ili kuhakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi na kuipa furaha familia kubwa ya Simba.