Safari ya Fiston Mayele: Kutoka Yanga Hadi Kufunga Kombe la Dunia 2026
KUNA mabao yanayofungwa na kusahaulika, lakini yapo yanayobeba ujumbe mkubwa zaidi kuliko matokeo ya mchezo.
Na sasa bao la Fiston Mayele dhidi ya Uzbekistan katika fainali za Kombe la Dunia 2026 ni miongoni mwa mabao yasiyosahaulika.
Kivipi? Twende taratibu utaelewa. Katika dakika ya 51, kocha wa DR Congo, Sébastien Desabre, alifanya uamuzi uliobadili mchezo huo.
Alimtoa Cedric Bakambu na kumuingiza Mayele wakati huo DR Congo ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 na ndoto za kufuzu hatua ya 32 Bora zilikuwa zimeanza kuyeyuka.
Dakika 39 baadaye, kila kitu kilikuwa kimebadilika, Yoane Wissa alisawazisha kwa penalti, Mayele akaifungia DR Congo bao la pili, kisha Wissa akahitimisha ushindi kwa bao la tatu.
DR Congo ikafuzu hatua ya mtoano huku jina la Mayele likiendelea kuandikwa katika historia ya kizazi hiki cha soka la DR Congo, lakini kwa Watanzania hasa mashabiki wa Yanga, simulizi hiyo ilianza miaka kadhaa iliyopita pale Jangwani.
YANGA ILIMPA NAFASI AFRIKA
Mayele hakuwasili Tanzania akiwa staa mkubwa, bali alikuja akitokea AS Vita ya DR Congo akiwa na sifa za mshambuliaji mzuri, ingawa hakuwa mchezaji ambaye kila mtu Afrika alikuwa akimzungumzia.
Ni ndani ya jezi ya Yanga ndipo jina lake lilipoanza kuvuka mipaka akiwafanya mabeki wa Ligi Kuu Bara kumheshimu huku akitetema kila ambapo alikuwa akicheka na nyavu, moja ya staili maarufu yake ya ushangiliaji.
Akaanza kuwatesa vigogo wa Afrika kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, ndiipo mawakala, makocha na klabu kubwa zikaanza kumfuatilia.
Kwa kifupi, Yanga haikumtengenezea kipaji, bali ilikipa fursa ya kuonekana Afrika nzima.
MSHAMBULIAJI WA MECHI KUBWA
Kitu kilichomtofautisha Mayele na washambuliaji wengi ni tabia yake ya kuamua mechi kubwa.
Hakuhitaji nafasi tano kufunga bao moja, alikuwa mshambuliaji ambaye wakati mwingine angegusa mpira mara chache ndani ya dakika 90 lakini akipewa nafasi moja tu, mara nyingi aliitumia.
Ndiyo maana alifunga mabao muhimu kwenye Kariakoo Derby, mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, akiiwezesha Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Mabao yake hayakuwa ya kupamba takwimu pekee, bali yaliyobadili historia ya Yanga.
TAKWIMU ZILIONGEA KULIKO MANENO
Katika misimu miwili aliyochezea Yanga, Mayele alijijengea sifa kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kuwahi kucheza Ligi Kuu Bara.
Alifunga mabao 33 kwenye ligi ambapo 16 alifunga msimu wa kwanza, 17 msimu wa pili. Pia alitwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu 2022/23 akilingana mabao (17) na Saido Ntibazonkiza aliyekuwa Simba.
Vilevile alifunga mabao 14 katika mashindano ya CAF, saba katika Ligi ya Mabingwa na saba kwenye Kombe la Shirikisho, ambapo alimaliza akiwa mfungaji bora wa michuano hiyo 2022/23.
Mbali na mabao hayo, alikuwa mhimili muhimu katika mafanikio ya Yanga kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho la Azam huku akiiongoza timu kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Takwimu na kiwango hicho ndicho kilichowavutia Pyramids FC ya Misri, ambayo haikusita kumsajili baada ya msimu wa 2022/23.
MAYELE NI YULEYULE
Wapo waliodhani mafanikio ya Mayele yalibaki Tanzania lakini alipojiunga na Pyramids FC aliendelea kufanya kilekile alichokuwa anakifanya Yanga.
Amefunga kwenye Ligi Kuu ya Misri, amefunga kwenye mashindano ya CAF, amefunga dhidi ya timu kubwa za Afrika, na sasa amefika mpaka Kombe la Dunia.
Hii inaonyesha jambo moja muhimu.
Ubora wake haukutokana na ligi aliyocheza, bali ulitokana na uwezo wake binafsi wa kusoma mchezo, kutafuta nafasi na kumalizia kwa utulivu.
UZITO WA BAO LAKE
Kufunga katika Kombe la Dunia si jambo la kawaida ni mashindano ambayo hata washambuliaji wakubwa duniani wamewahi kuyamaliza bila kufunga hata bao moja.
Lakini, Mayele ameingia akitokea benchi na kutumia nafasi yake kwa ukamilifu, bao lake dhidi ya Uzbekistan halikuipa Congo ushindi pekee, bali lilikuwa bao lililoivusha nchi yake kwenda hatua ya mtoano.
Hayo ndiyo mabao ambayo washambuliaji hukumbukwa nayo kwa miaka mingi.
WISSA NA MAYELE
DR Congo imepata silaha mpya katika safu yake ya ushambuliaji, Yoane Wissa analeta kasi, nguvu na uwezo wa kushambulia kutoka maeneo mapana ya uwanja.
Mayele analeta utulivu, akili ya kutafuta nafasi na umaliziaji wa kiwango cha juu dhidi ya Uzbekistan, wawili hao walionyesha jinsi wanavyoweza kubadilisha mchezo ndani ya dakika chache.
Ni ushirikiano ambao unaweza kuisumbua timu yoyote katika hatua ya 32 Bora.
VIPI KUHUSU YANGA?
Je! Yanga imepoteza mshambuliaji bora zaidi katika historia yake? mjadala huo unaweza kushika kasi kutoka na mafanikio yake kadiri anavyopiga hatua.
Lakini, ukweli mmoja hauwezi kupingwa, Mayele ameondoka Yanga, akaenda Misri na sasa anafunga kwenye Kombe la Dunia bila kupoteza utambulisho wake kama mshambuliaji mwenye uwezo wa kuamua mechi.
Ni ushahidi kuwa kiwango alichokionyesha Tanzania hakikuwa cha bahati mbaya, kilikuwa ni mwanzo wa safari ya mshambuliaji ambaye leo anasimama kwenye michuano mikubwa zaidi ya soka duniani.
Kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa hadi viwanja vya Kombe la Dunia, safari ya Fiston Mayele imekuwa somo kwamba Afrika ina vipaji vinavyoweza kushindana na dunia.
Na kwa mashabiki wa Yanga, kila bao analofunga leo linaendelea kukumbusha siku ambazo alikuwa shujaa wao Jangwani.