LICHA ya kuwepo kwa maneno yanayohoji kushuka kwa kiwango cha nyota wa Simba, Elie Mpanzu, bado takwimu zinaonyesha wazi mchango wake mkubwa ndani ya kikosi hicho msimu huu.
Kiungo huyo amehusika moja kwa moja katika mabao matano ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akifunga mawili na kutoa pasi tatu za mabao, jambo linaloonesha kuwa bado ni silaha muhimu kwa timu hiyo.
Mpanzu amecheza jumla ya dakika 516, sawa na takribani mechi tano na dakika 66, ndani ya michezo 11 aliyopata nafasi ya kucheza hadi sasa, akionesha uthabiti wa kiwango chake licha ya changamoto alizokutana nazo.
Pamoja na kupitiwa na kipindi kigumu kilichohusisha changamoto za kifamilia, bado amekuwa na mchango chanya uwanjani, akijitahidi kila anapopata nafasi ya kuisaidia timu yake.
Ubora wake unaonekana si tu kwenye kufunga na kutengeneza mabao, bali pia katika namna anavyochangia uchezaji wa timu kwa ujumla, hasa katika eneo la kiungo.
Kutokana na mwenendo huo, kocha wa Simba, Steve Barker ameendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kucheza, iwe ni kuanza kikosi cha kwanza au kuingia akitokea benchi.
Imani hiyo ya benchi la ufundi imeendelea kumjenga Mpanzu kurejea kwenye kiwango chake bora, huku akionekana kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuleta tofauti katika harakati za Simba kusaka mafanikio msimu huu.