KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, ameeleza kuwa timu yao ina ari ya ushindi kila mechi, matokeo ya jana hayakikidhi matarajio yao. Sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba ilibaki kikwazo kidogo katika jitihada zao za kupata pointi tatu kila mechi.
Barker amesema sare hiyo haikuwa matokeo waliyoyatarajia, kwani kila wanapoingia uwanjani, lengo kuu ni kushinda.
“Tunapoanza mchezo, kila kitu kinaelekezwa kupata pointi tatu. Leo hatukufanikisha hilo, lakini tunajua changamoto ni sehemu ya mpira,” amesema kocha huyo.
Kocha huyo ameongeza kuwa walijua mapema kuwa mechi hiyo usingekuwa rahisi. Pamba ni timu imara yenye changamoto kubwa kwa wapinzani.
“Kabla ya mchezo, walikuwa wamepoteza michezo mitatu pekee, jambo linaloonesha nguvu na ubora wa kikosi chao. Tayari walionesha uwezo wao dhidi ya Azam, jambo lililotufanya Simba kuongeza jitihada, hasa kwenye eneo la ushambuliaji la mwisho,” ameeleza Barker.
Pamoja na changamoto hizo, Barker amesema Simba ilihitaji usahihi zaidi na ubunifu ili kufanikisha kupata matokeo chanya.
Hali hiyo ilizidishwa na kukosekana kwa baadhi ya washambuliaji kutokana na majeraha na adhabu za kusimamishwa, jambo lililolazimisha kufanya mabadiliko kwenye kikosi. Hii ililenga kuongeza nguvu na tija mbele ya lango la mpinzani.
Licha ya kutoridhishwa na sare hiyo, kocha Barker amesisitiza kuwa kuna dalili nzuri zinazonyesha timu ipo kwenye mwelekeo sahihi na ina kasi nzuri ya maendeleo.
“Sare hii ni kikwazo kidogo tu, sehemu ya safari yetu kuelekea malengo makuu ya msimu. Sasa tunaangalia michezo miwili ya nyumbani inayofuata,” amesema.
Barker amesema jambo muhimu zaidi ni namna timu itakavyojibu baada ya matokeo haya. Kila nafasi ni muhimu kuhakikisha Simba inabaki kwenye hali ya ushindi, huku wakiendelea kujenga mwelekeo mzuri wa ushindani msimu huu.