Memphis Depay Aipaka Bope Corinthians: “Wamekiuka Makubaliano Yard”
Aliyewahi kuwa mshambuliaji wa Manchester United na raia wa Uholanzi, Memphis Depay, ameibuka na kukosoa vikali uongozi wa klabu ya Corinthians ya Brazil kwa kuamua kutomwongezea mkataba mpya, akisisitiza kuwa klabu hiyo imekiuka makubaliano rasmi waliyofikia.
Hivi karibuni, Corinthians ilithibitisha rasmi kuwa haitakuwa na mpango wa kurefusha mkataba wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 32. Kulingana na taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake São Paulo, uamuzi huo umechukuliwa ili kulinda na kuimarisha ukwasi pamoja na hali ya kifedha ya klabu.
Hata hivyo, taarifa hiyo imeonekana kumkera Depay ambaye ameweka wazi kuwa pande zote mbili tayari zilikuwa zimefikia muafaka wa kuongeza mkataba wa miaka miwili zaidi. Depay aliongeza kuwa mpango huo wa mkataba mpya ulikuwa umeshaidhinishwa na rais wa klabu pamoja na idara zote muhimu ikiwemo za michezo, sheria na fedha.
Kutokana na hatua hiyo, mshambuliaji huyo ameishutumu Corinthians kwa kile alichokiita “tabia isiyokubalika” na kuonyesha nia ya kuchukua hatua za kisheria ili kulinda maslahi yake.
Akieleza hisia zake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), Depay aliandika:
“Nimekatishwa tamaa sana kusoma kwamba Corinthians imeamua kutoheshimu makubaliano tuliyokuwa tumefikia ya kuongeza mkataba wangu kwa miaka miwili zaidi.
Makubaliano hayo yalikuwa yamepitishwa wazi na rais pamoja na idara za michezo, sheria na fedha. Hata hivyo, baadhi ya watu wameamua kukiuka makubaliano hayo.
Sikutaka hali hii itokee na wakati wote nimeiheshimu klabu katika mchakato huu, lakini sasa ninalazimika kuchukua hatua kali ili kulinda maslahi yangu. Katika siku zijazo nitaeleza hadharani kuhusu suala hili, lakini msione shaka kwamba sitaruhusu tabia hii isiyokubalika ipite bila kuchukua hatua.”
Mzozo huu unaashiria mwisho wa safari ya Depay ndani ya klabu hiyo ya Brazil baada ya kuitumikia kwa takribani miaka miwili tangu alipojiunga nayo akitokea barani Ulaya. Mshambuliaji huyo alitazamiwa kuwa nguzo kuu ya kikosi hicho, lakini sasa lazima atafute changamoto mpya huku mzozo wa mkataba wake ukichukua sura mpya.