Simba SC usajili mpya
Simba SC

Ahmed Ally Afunguka Usajili Mpya Simba SC: Bado Maboresho Mengine Yanakuja!

Vardo August 13, 2026 2:13 pm

BAADA ya kukamilika kwa mechi za Ngao ya Jamii, klabu ya Simba SC imeweka pembeni matokeo hayo na sasa nguvu zote zimeelekezwa kwenye mbio za Ligi Kuu ya NBC (Bara), huku uongozi ukianza kufanyia kazi maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amebainisha kuwa kila idara ndani ya klabu hiyo ipo tayari kutimiza wajibu wake. Uongozi tayari umeanza mchakato wa kuziba mapungufu yote yaliyoonekana ili kuhakikisha kikosi kinakuwa imara zaidi.


Macho na Akili Kwenye Mchezo Dhidi ya Kagera Sugar

Ahmed Ally amesisitiza kuwa kwa sasa akili zote za Msimbazi zipo kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, na tayari maandalizi ya safari ya kuelekea mkoani Kagera yameanza rasmi.

Simba inatarajiwa kutua mkoani Kagera Agosti 15 tayari kwa pambano hilo. Afisa habari huyo amesisitiza umuhimu wa kuanza msimu mpya kwa ushindi ili kukusanya alama zote tatu muhimu mapema.

“Agosti 15 tutaenda Kagera kwa ajili ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar. Tumeanza kutazama mechi ya Kagera ili tusipoteze pointi. Kila Mwanasimba tushikamane ili tupate alama tatu katika mechi hii ya ligi,” alisema Ahmed Ally.


Uongozi Waanza Kazi Ya Maboresho Kwenye Kikosi

Akizungumzia kuhusu uwezekano wa kuongeza wachezaji wengine kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, Ahmed ametoa ishara njema kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kwa kueleza kuwa viongozi tayari wapo kazini.

“Viongozi kama kuna sehemu ya usajili inatakiwa kufanyiwa kazi, basi kuanzia jana wameanza kuyafanyia kazi maeneo hayo,” aliongeza Ahmed Ally.

Kauli hii imeleta matumaini makubwa kwa mashabiki wa Simba ambao wanatamani kuona wachezaji wengine wapya wakitambulishwa ili kuimarisha maeneo yenye changamoto.

Kwa sasa, lengo kuu la Wekundu wa Msimbazi ni kuanza ligi kwa kishindo na kusahau matokeo ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao Yanga SC, huku mchezo dhidi ya Kagera Sugar ukiwa mtihani wa kwanza kabisa wa kikosi hicho.

Yanga Yafunguka Ofa Za Wydad na FAR Rabat Mkononi: Hatima ya Allan Okello Hii Hapa! Steve Barker Aanza Kazi Simba SC: Afanya Mabadiliko Makubwa Ushambuliaji Baada ya Kipigo cha Yanga