Taifa Stars dhidi ya Madagascar
Taifa Stars

Taifa Stars vs Madagascar Leo: Rekodi na Mambo 5 Yanayoipa Stars Jeuri ya Ushindi!

Vardo September 29, 2026 10:31 am

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) leo inashuka dimbani kumenyana na Madagascar katika mchezo wa Kundi L wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027). Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa d’Honneur, Meknes nchini Morocco kuanzia saa 10:00 jioni kwa majira ya Tanzania.

Mchezo huu unakuja ikiwa ni siku chache tangu Taifa Stars ianze vibaya kampeni hiyo kwa kukubali kichapo cha mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Guinea-Bissau. Matokeo hayo yanaongeza umuhimu mkubwa kwa Stars kusaka ushindi leo ili kurejesha hali ya kujiamini.

Rekodi ya Heshima: Taifa Stars Inaiweka Madagascar Chini

Kabla ya kuingia uwanjani, Taifa Stars ina kila sababu ya kujivunia historia ya michezo yake dhidi ya Madagascar. Timu hizi zimekutana mara 10 katika mashindano rasmi:

  • Ushindi kwa Taifa Stars: Mara 4

  • Sare: Mara 3

  • Ushindi kwa Madagascar: Mara 3

Ingawa Madagascar inaongoza kwa idadi ya mabao ya kufunga (mabao 17 dhidi ya 15 ya Stars), Tanzania ndiyo inayoshikilia idadi kubwa ya ushindi katika mikutano yao rasmi.

Historia ya Mechi Zao za Nyuma

  • Michezo ya Afrika (1965): Madagascar ilianza kwa ushindi wa mabao 5-1, lakini Stars ikajibu mapigo siku mbili baadaye kwa ushindi wa mabao 2-1.

  • Kufuzu Olimpiki (1967): Madagascar ilitawala kwa kuifunga Tanzania mabao 4-2 na 2-0.

  • Kufuzu Kombe la Dunia: Taifa Stars haijawahi kupoteza dhidi ya Madagascar kwenye michuano hii. Mwaka 1992 zilitoka 0-0, na mwaka 2021 Stars ilishinda 3-2 nyumbani kabla ya kutoka sare ya 1-1 ugenini.

  • Mechi za Karibuni (2025): Juni 2025, Madagascar ilishinda 1-0 kwenye COSAFA, lakini Stars ikalipa kisasi mwezi Agosti kwa ushindi wa mabao 2-1 katika michuano ya CHAN.

Kauli ya Kocha Miguel Gamondi

Akimzungumzia mchezo wa leo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amebainisha kuwa pamoja na muda kuwa mchache, kikosi kipo tayari kutoa muunganiko mzuri.

“Hakuna muda mwingi wa kubadili mambo, hivyo tutaendelea na mfumo wetu na kujaribu kuboresha. Nadhani tupo kwenye njia sahihi ya kujenga timu hii kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zijazo,” alisema Gamondi.

Tiketi ya AFCON 2027 Mkononi

Zaidi ya yote, matokeo ya mchezo wa leo hayataondoa nafasi ya Taifa Stars kushiriki AFCON 2027, kwani tayari Tanzania inayo tiketi ya moja kwa moja kama nchi mwenyeji wa michuano hiyo ikishirikiana na Kenya pamoja na Uganda.

Hata hivyo, ushindi wa leo ni fursa mhimu kwa Stars kuongeza ushindi wake wa 5 dhidi ya Madagascar na kuendeleza ubora wake wa kihistoria.

Clement Mzize Atoa Onyo Zito Ligi Kuu: “Wasubiri Kuona Mara Mbili Yake”