Yanga vs Simba Ngao ya Jamii: Mfumo Mpya wa Video Support (FVS) Kutumika Leo
Nchi inasimama! Itakapotimia saa 2:30 usiku wa leo, macho na masikio ya wapenda soka wote yatakuwa katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, ambapo miamba ya soka la Bongo, Yanga SC na Simba SC, itazipiga katika Mchezo wa Dabi ya Kariakoo kuwania taji la Ngao ya Jamii 2026.
Mchezo huu wa ufunguzi wa pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuwa wa vuta-nikuvute, kwani kila timu inasaka ubingwa wa kwanza wa msimu ili kuanza kwa kishindo.
Waamuzi wa Mchezo Wawekwa Wazi
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemteua mwamuzi Ahmed Arajiga kuwa Mwamuzi wa Kati katika pambano hili kubwa. Arajiga atasaidiwa na waamuzi wa pembeni:
-
Mohammed Mkono (Mwamuzi Msaidizi wa Kwanza)
-
Leonard Mkumbo (Mwamuzi Msaidizi wa Pili)
-
Nassir Siyah (Mwamuzi wa Mezani / Fourth Official)
Historia Kuandikwa: Mfumo Mpya wa Video Support (FVS) Kutumika
Mchezo wa leo unaingia kwenye historia ya soka nchini kwa kuwa wa kwanza kutumia mfumo wa Video Support (FVS), ambao utawasaidia waamuzi kupitia upya matukio ya utata uwanjani.
Tofauti na mfumo wa VAR unaotumiwa na waamuzi pekee kufanya maamuzi kutoka chumba maalum, mfumo huu wa Video Support unatoa fursa kwa mabenchi ya ufundi ya timu husika kuomba marudio ya matukio.
1. Video Support Inatumikaje Uwanjani?
-
Kadi Mbili Maalum: Kila timu (Yanga na Simba) itapewa kadi mbili maalum zitakazowekwa kwenye benchi la ufundi.
-
Jukumu la Kocha Mkuu: Endapo timu itaona kuna tukio la utata uwanjani (mfano: Penalti, Kadi Nyekundu, au Golini), Kocha Mkuu pekee ndiye mwenye mamlaka ya kwenda kwa mwamuzi wa kati akiwa na kadi hiyo kuomba tukio lirudiwe.
-
Uamuzi wa Mwamuzi: Mwamuzi atenda kwenye skrini iliyo pembezoni mwa uwanja kutazama marudio ya picha za video kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.
2. Hatma ya Kadi na Kanuni Zake
-
Ombi Likikubaliwa: Kama mwamuzi akitazama video na kubaini timu ilikuwa sahihi na haikutendewa haki, atatangaza maamuzi mapya kwa uwanja mzima na kadi hiyo itarudishwa kwa kocha. Timu itaendelea kuwa na nafasi zake za kuomba tena.
-
Ombi Likikataliwa: Kama mwamuzi akijiridhisha kuwa maamuzi ya mwanzo yalikuwa sahihi, kadi hiyo itachukuliwa na timu husika itabakiwa na kadi moja pekee.
-
Kadi Zikimalizika: Endapo timu itaomba marudio mara mbili na yote yakagundulika hayakuwa na makosa, itakuwa imepoteza fursa zote na mchezo utaendelea bila uwezo wa kuomba marudio mengine.
Lengo kuu la kanuni hii ni kuzuia mabenchi ya ufundi kupoteza muda au kuomba marudio bila sababu za msingi.
Maandalizi ya Mitambo na Wataalamu kutoka Nje
Katika kuhakikisha huduma hii inafanya kazi bila hitilafu:
-
Wataalamu sita (6) raia wa kigeni wamewasili Uwanja wa Amaan kusimamia na kufunga mitambo hiyo kwenye chumba maalum.
-
Mtambo huo utatumia picha za video kutoka kwenye matangazo ya moja kwa moja (Live Broadcast).
-
Mwamuzi wa kati amewekewa TV maalum pembezoni mwa uwanja kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi.
Je, ni timu gani itaondoka na taji la kwanza la Ngao ya Jamii msimu huu? Nini maoni yako kuhusu matumizi ya mfumo huu mpya wa Video Support? Tumia sehemu ya maoni hapo chini kutoa maoni yako!