Wasanii wa Bongo Flava
Burudani

Mastaa 10 wa Bongo Flava na Wasanii wa Nje Waliowavutia

Vardo September 27, 2026 10:55 am

Kupitia mahojiano mbalimbali, baadhi ya mastaa wakubwa wa Bongo Flava wamewahi kuwataja wasanii kutoka nje ambao wanawashabikia au waliowavutia hadi na wao kuamua kuingia kwenye kiwanda cha muziki.

Wanamuziki nguli duniani kama Celine Dion, Michael Jackson na Beyoncé wamekuwa chachu na mfano wa kuigwa kwa wasanii wengi wanaochipukia. Hapa tunakuangazia mastaa 10 wa Bongo Flava na sanamu zao za kimuziki kutoka nje ya nchi:

1. Diamond Platnumz – Usher Raymond

Kipindi akiwa na ndoto ya kuja kuwa mwanamuziki mkubwa, msanii aliyemvutia zaidi Diamond Platnumz na kumtazama kama mfano wa kuigwa ni Usher Raymond IV. Usher ni mshindi wa tuzo nane za Grammy aliyepata umaarufu mkubwa mwishoni mwa miaka ya 1990 kupitia albamu yake ya My Way (1997).

2. Vanessa Mdee – Alicia Keys na Whitney Houston

Waimbaji wa kike mashuhuri duniani kama Alicia Keys, Whitney Houston, Lauryn Hill, Toni Braxton, Celine Dion, Monica, Destiny’s Child, Aaliyah, Mary J. Blige na Mariah Carey, ndio waliompa hamasa Vanessa Mdee kuingia kwenye muziki kabla ya kutangaza kustaafu.

3. K-Lynn – Mariah Carey na Whitney Houston

Mshindi huyu wa Miss Tanzania 2000 anaeleza kuwa tangu akiwa mdogo alikuwa akitazama video za Mariah Carey na Whitney Houston wakiimba mubashara (live), na kutamani siku moja kufikia viwango vyao. Ni hamasa hiyo iliyomfanya afanye vizuri kupitia kibao chake cha Nalia kwa Furaha na nyimbo zingine zilizohiti.

4. Banana Zorro – Michael Jackson

Kabla ya kuibuka mshindi wa Tanzania Pop Idol 2001, tayari Banana Zorro alikuwa akijifunza mengi kutoka kwa Mfalme wa Pop, Michael Jackson—mwanamuziki aliyetawala chati za dunia na kuuza zaidi ya rekodi milioni 400.

5. AY – Dr. Dre

Mwanachama huyu wa zamani wa East Coast Team ni shabiki mkubwa wa mtayarishaji na mwanamuziki Dr. Dre. AY alishawahi kueleza kuwa moja ya ndoto zake kubwa ilikuwa ni kukutana na kufanya kazi na Bosi huyo wa Aftermath Entertainment, inayowasimamia wasanii kama Eminem na Kendrick Lamar.

6. Lady Jaydee – Rihanna

Baada ya kizazi cha Whitney Houston, mwanamuziki Lady Jaydee anamtaja Rihanna kama mwanamuziki aliyemvutia zaidi miaka ya hivi karibuni. Jaydee anasema amekuwa akizipa maksi 100% melodi na uimbaji wa Rihanna.

7. Sugu – Jay-Z

Mkongwe huyu wa rap nchini ni shabiki mkubwa wa Jay-Z kiasi cha kuamua kumpa mtoto wake wa kwanza wa kiume jina la Shawn—ambalo ndilo jina halisi la Jay-Z (Shawn Corey Carter).

8. Lulu Diva – Beyoncé na Celine Dion

Licha ya kuanzia kwenye tasnia ya uigizaji, ndoto kubwa ya Lulu Diva ilikuwa ni kufanya muziki. Wasanii waliompa msukumo wa kutimiza ndoto hiyo ni pamoja na Celine Dion na Beyoncé Knowles.

9. Shaa – Aaliyah na Brandy

Kabla ya kuweka rekodi kama msanii wa kwanza wa kike kusainiwa chini ya lebo ya MJ Records, Shaa alivutiwa sana na waimbaji kama Aaliyah, Brandy, Toni Braxton na Madonna, kufuatia dada yake kuwa akisikiliza nyimbo zao mara kwa mara.

10. Dudu Baya – 2Pac na DMX

Alianza muziki mwaka 1999, na wakali waliompa ushawishi mkubwa ni 2Pac na DMX waliotamba sana miaka ya 1990. 2Pac aliteka hisia zake kupitia albamu ya All Eyez on Me (1996), huku DMX akimvutia kupitia albamu ya It’s Dark and Hell Is Hot na ngoma ya Party Up.

Je, D Voice Ni Mfalme wa Singeli Au Anaitumia Tu Kama Kichaka? Ukweli Unasikitisha! Hamad Ubwa ‘Baro’: Nataka Kutwaa Tena Tuzo ya Kipa Bora Ligi Kuu Zanzibar