Je, D Voice Ni Mfalme wa Singeli Au Anaitumia Tu Kama Kichaka? Ukweli Unasikitisha!
Kila mara mwanamuziki D Voice anapojitambulisha, amekuwa akijinasibu kama msanii wa Singeli. Hata hivyo, mtindo wake wa kufanya muziki tangu alipojiunga na lebo ya WCB Wasafi umeacha maswali mengi na kumweka mbali na ufalme wa Singeli ambao anazidi kujivika.
Kabla ya kutambulishwa na WCB Wasafi mwaka 2023, D Voice alikuwa akifanya Singeli kwa asilimia 100. Wimbo wake uliompa umaarufu mkubwa ulikuwa ni ‘Kuachana Shingapi’ (2021), ambao baadaye alifanya remix akiwashirikisha Barnaba, Lody Music na Platform. Lakini baada ya kuingia WCB, uzito wake katika muziki wa Singeli umeshuka hadi kufikia asilimia 20 tu.
Ukweli Kuhusu Rekodi za D Voice na WCB Wasafi
Hivi karibuni, WCB Wasafi ilitaja rekodi mbalimbali za D Voice ili kuonyesha ukubwa wake katika muziki wa Singeli. Rekodi hizo ni pamoja na:
-
Kuwa msanii namba moja wa Singeli mwenye subscribers wengi zaidi YouTube.
-
Kuwa msanii wa Singeli mwenye nyimbo zilizosikilizwa au kutazamwa zaidi (most streamed) kwenye majukwaa ya digitali kama YouTube na Boomplay.
Hata hivyo, ukizichunguza rekodi hizi kwa umakini, utagundua kuwa D Voice na lebo yake wanatumia mafanikio ya Bongo Fleva ili kupora Ufalme wa Singeli.
Takwimu Za Nyimbo Zake Za Mwaka 2026
Tangu kuanzia mwezi Januari hadi Septemba 2026, D Voice ameachia jumla ya nyimbo tano (5):
-
Ningepata Nafasi (Bongo Fleva)
-
Baridi ft. Zuchu (Bongo Fleva)
-
Iyo ft. Diamond Platnumz (Singeli)
-
Kumbe (Bongo Fleva)
-
Banana ft. Jay Melody (Bongo Fleva)
Kati ya nyimbo hizi tano, ni wimbo mmoja tu (Iyo) ndio wa Singeli! Hii ina maana kwamba kwa mwaka huu, asilimia 80 ya kazi zake ni za Bongo Fleva na ni asilimia 20 pekee ndizo za Singeli.
Hapa ndipo swali linapokuja: Je, inakuaje msanii aliyetoa wimbo mmoja tu wa Singeli kwa mwaka mzima akae kundi moja na wasanii kama Dulla Makabila walioachia kazi nyingi za Singeli?
Albamu ya ‘Swahili Kid’ na Consequence Kwenye YouTube
Ukiangalia albamu yake ya kwanza ya Swahili Kid (2023) yenye nyimbo 10, ni nyimbo 4 pekee zilizokuwa za Singeli (sawa na 40%). Nyimbo zilizofanya vizuri zaidi na kupata maelfu ya views zilikuwa za Bongo Fleva, mfano ‘BamBam’ akiwa na Zuchu uliopata zaidi ya views milioni 25.
Pia, wimbo wake uliotazamwa zaidi YouTube mpaka sasa ni ‘Tunapendana’ (2024) aliyomshirikisha Mbosso wenye zaidi ya views milioni 38—na huo ni wimbo wa Bongo Fleva.
Kwa ujumla:
-
Nyimbo 11 za Bongo Fleva za D Voice: Zimejikusanyia zaidi ya views milioni 148.7 YouTube.
-
Nyimbo zake zote za Singeli: Hazijafikisha hata views milioni 10 kwa pamoja.
Hukumu ya Mwisho: Singeli Kama Kichaka Cha Kujifichia
Kwa takwimu hizi, ni wazi kwamba mashabiki na namba za kidijitali zinamweka D Voice kwenye kundi la wasanii wa Bongo Fleva na sio Singeli.
D Voice na WCB Wasafi wamechagua kuutumia muziki wa Singeli kama kichaka cha kuchukulia mataji na ufalme ambao anajua ni vigumu kuupata kirahisi kwenye Bongo Fleva kutokana na ushindani mkubwa uliopo. Ni muda sasa wa D Voice kukubali matokeo na kujitambulisha rasmi kama msanii wa Bongo Fleva!