Habari za michezo

Paul Pogba Kuondoka Monaco? Ukweli Kuhusu Mkataba Wake

Vardo August 12, 2026 3:11 pm

MONACO, Ufaransa — Kiungo wa kimataifa wa Ufaransa na mshindi wa Kombe la Dunia 2018, Paul Pogba, yuko mbioni kusitisha mkataba wake na klabu ya AS Monaco mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Pogba (32), alijiunga na Monaco msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili mara baada ya kurejea uwanjani kufuatia kifungo cha miezi 18 kutokana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Hata hivyo, safari yake ndani ya Monaco imekumbwa na changamoto kubwa za majeraha ya mara kwa mara, hali inayoweka rehani siku zake za usoni klabuni hapo.

Mabadiliko ya Kocha na Ushindani wa Namba Mbali na majeraha, mabadiliko ya benchi la ufundi pia yamechangia sintofahamu ya namba yake klabuni hapo. Baada ya Kocha Filipe Luis kuchukua mikoba ya Sebastien Pocognoli, mfumo mpya wa timu umeongeza ushindani mkali katika eneo la kiungo cha kati.

Kutoka Miaka 4 Mpaka Miezi 18 Ikumbukwe kuwa Pogba awali alitakiwa kutumikia adhabu ya kufungiwa soka kwa miaka minne mwaka 2023. Hata hivyo, baada ya kukata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), adhabu hiyo ilipunguzwa hadi miezi 18, hatua iliyomruhusu kurejea uwanjani Machi 2025.

Kwa sasa, uongozi wa Monaco haujatoa tamko rasmi kuhusu kuvunjwa kwa mkataba wake. Hata hivyo, vyanzo vya karibu vinaeleza kuwa Pogba anasubiri matokeo ya vipimo vya kina kutoka kwa timu ya madaktari ili kubaini ukubwa wa jeraha alilopata hivi karibuni mazoezini kabla ya kuchukua hatua ya mwisho.

PSG Kuisaka Rekodi ya Real Madrid Ligi ya Mabingwa Ulaya