Home Habari za michezo IBENGE AFUNGUKA, MBINU MPYA ZAIOKOA AZAM MBELE YA SIMBA

IBENGE AFUNGUKA, MBINU MPYA ZAIOKOA AZAM MBELE YA SIMBA

0

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amefunguka kufuatia sare ya bila kufungana dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ibenge amesema timu yake ilikumbana na changamoto kubwa katika kipindi cha kwanza, ambapo Simba walionekana kuwa bora zaidi kwa kutawala mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, ingawa walishindwa kuzitumia ipasavyo.

Kocha huyo ameweka wazi kuwa mabadiliko ya mbinu pamoja na kuongezeka kwa morali kwa wachezaji wake kulichangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa Azam FC katika kipindi cha pili, ambapo walirejea uwanjani wakiwa na kasi na ushindani mkubwa zaidi.

“Licha ya changamoto tulizokutana nazo mwanzoni, tulirejea kwa nguvu kipindi cha pili na kuonesha kiwango bora zaidi kilichotupa nafasi ya kushindana sawasawa na wapinzani wetu,” amesema Ibenge.

Ameongeza kuwa mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa na wa kuvutia, huku kila timu ikipambana kwa juhudi kutafuta ushindi, jambo lililofanya pambano hilo kuwa la kiwango cha juu licha ya kumalizika bila mabao.

Ibenge  ameeleza kuridhishwa na mwitikio wa wachezaji wake baada ya mapumziko, akisisitiza kuwa benchi la ufundi litaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza ili kuhakikisha timu inapata matokeo bora zaidi katika michezo ijayo.