Home Habari za michezo SIMBA YASUBIRI RATIBA KWA JEURI, YAAPA KUVUNJA REKODI ROBO FAINALI

SIMBA YASUBIRI RATIBA KWA JEURI, YAAPA KUVUNJA REKODI ROBO FAINALI

0

MENEJA  wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, amesema kuwa kwa sasa kikosi hicho kinasubiri kwa hamu ratiba rasmi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ili kufahamu kitapambana na nani na lini.

Amesema  kati ya timu saba zilizokwisha fuzu hatua hiyo, pamoja na Simba kukamilisha idadi ya timu nane, wao wapo tayari kukutana na mpinzani yeyote watakayepangwa naye.

Ameongeza kuwa kauli hiyo wanaitoa kwa kujiamini kutokana na ubora wa kikosi chao na kiwango wanachoonyesha uwanjani kwa sasa.

“Simba ina uwezo wa kucheza na kupata matokeo mbele ya timu yoyote, bila kujali ukubwa wa mpinzani,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa wanaendelea kujivunia ushindi walioupata dhidi ya Dodoma Jiji huku wakigeukia maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Fountain Gate, ambao nao unaonekana kuwa na ushindani mkubwa.

Amesema  kadri ligi inavyoelekea hatua za mwisho, kila mechi inakuwa ngumu na yenye presha kubwa, hivyo ni muhimu kwa wachezaji kuendelea kuwa makini na kupambana ili kupata matokeo chanya.

Akizungumzia mchezo ujao, Ahmed amesema kesho jumatano  kikosi kina kibarua kizito dhidi ya Fountain Gate FC, na ametoa wito kwa mashabiki wa Simba, hususan wa Kanda ya Kaskazini, kuendelea kuisapoti timu yao ili kumaliza vizuri sehemu iliyobaki ya msimu.

Amesisitiza kuwa nguvu na morali waliyoionyesha katika michezo dhidi ya TRA United na Dodoma Jiji inapaswa kuhamishiwa kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate, kwa lengo la kuvuna alama tatu muhimu kabla ya kuikabili Namungo FC katika mechi inayofuata.