Home Habari za michezo SIMBA YAVUNA MABAO 6-0 FOUNTAIN GATE

SIMBA YAVUNA MABAO 6-0 FOUNTAIN GATE

0

KATIKA mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu baina ya Simba dhidi ya Fountain Gate, yamezalishwa mabao sita ambayo yote yamefungwa na Wekundu wa Msimbazi.

Duru la kwanza Septemba 25, 2025 Simba ikiwa mwenyeji kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ilishinda 3-0 kupitia mabao ya Rushine De Reuck dakika ya sita, Jean Charles Ahoua (dk 37) na Jonathan Sowah (dk 58). Leo Aprili 15, 2026, Simba ikashinda tena 3-0 wafungaji wakiwa Clatous Chama (dk 45+6), Libase Gueye (dk 53) na Shaban Pandu aliyejifunga dakika ya 71.

Ushindi huo wa Simba leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, umekuja baada ya dakika 180 ‘ngumu’ bila ya bao katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara.

Awali Simba ilikumbana na wakati mgumu katika mechi mbili zilizopita kufuatia kushindwa kufunga bao mbele ya Azam, April 5, 2026 huko Chamazi na TRA United siku nne baadaye (April 9) zote ikiwa ugenini na kujikuta ikidondosha pointi nne.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Simba msimu huu kucheza dakika 180 bila ya bao, mara ya kwanza ilikuwa Februari, 2026 ilifanya hivyo dhidi ya Dodoma Jiji na Yanga kwenye Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Zanzibar.

MECHI ILIVYOKUWA

Simba ilizianza dakika 45 za mchezo huo ikionekana kuwa na papara katika eneo la mwisho la ushambuliaji ambalo lilikuwa likiongozwa na Selemani Mwalimu mwenye mabao sita Ligi Kuu, jambo lililowafanya Fountain Gate kuhimili presha yao ya mashambulizi katika dakika 30 za kipindi cha kwanza.

Wakati ambao Fountain Gate wakiamini wanaweza kwenda mapumziko wakiwa wameizuia Simba kupata bao katika dakika 45 za kipindi cha kwanza ndipo Mwamba wa Lusaka, Clatous Chama alipoachia mkwaju katika dakika za nyongeza (45+6) uliomshinda Machupa Kapili na kufunga bao lake la kwanza msimu huu katika ligi akiwa na uzi wa Wekundu hao wa Msimbazi.

Baada ya kuwa mbele kwa bao 1-0, Simba ilirejea kipindi cha pili na kuonekana kuwa na utulivu zaidi katika eneo la mwisho, jambo lililowafanya vijana hao wa Steve Barker kupata bao la pili katika dakika ya 53 ambalo lilifungwa na Libasse Gueye kufuatia asisti ya Seleman Mwalimu.

Katika dakika ya 65, Simba ilifanya mabadiliko mawili kwa mpigo ikiwa ni mabadiliko yao ya tatu katika mchezo huo, walitolewa Mwalimu na Clement Kibabage huku wakiingia Anthony Mligo na Elie Mpanzu, awali aliingia Inno Loemba kuchukua nafasi ya Neo Maema.

Wakati Simba ikiwa mbele kwa mabao hayo, iliendelea kucheza kwa kujiamini huku ikitengeneza presha kubwa zaidi ya mashambulizi ambayo ilizaa matunda na kupata bao la tatu ambalo Shabani Pandu alijifunga.

Baada ya kuwa mbele kwa mabao 3-0, Barker aliamua kufanya mabadiliko mengine mawili kwa mpigo kwa kuwapa nafasi ya Hussein Mbegu na Morice Abraham wakichukua nafasi ya Rushine De Reuck na Chama.

Matokeo hayo yameifanya Simba ambayo imeendelea kuwa nafasi ya pili ikiwa na pointi 39 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, kupunguza tofauti ya pointi kati yao na vinara, Yanga kutoka nane hadi tano.

DOZI YA BAO TATU

Ushindi wa mabao 3-0 ambao Simba imeibuka nao huko Arusha ni wa tano msimu huu kwa Mnyama katika mfululizo wa mechi zake za Ligi Kuu Bara huku kikiwa kipigo cha pili kwa Fountain Gate FC ndani ya msimu mmoja.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Fountain Gate FC ilichapwa mabao 3-0 kama ilivyokuwa jana na Simba, mechi nyingine ambazo Mnyama amepata ushindi wa namna hiyo ni dhidi ya TRA, Mbeya City na Namungo. Ushindi wa mabao 3-0, ndio mkubwa zaidi kwa Simba msimu huu wa Ligi Kuu Bara.