WABURUZA mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, KMC, hali yao sio nzuri huku wakiendelea kupambana kuepuka kushuka daraja.
Katika mapambano hayo, Aprili 14, 2026, timu hiyo ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons na kupata pointi moja baada ya kupita siku 70 ambazo ni sawa na miezi miwili na siku 11.
Tanzania Prisons ilikuwa ya kwanza kupata bao katika mechi hiyo likifungwa na Jeremiah Juma dakika ya tano, kisha wenyeji KMC wakasawazisha dakika ya 38, mfungaji akiwa Adam Uledi.
KMC kabla ya sare hiyo, mara ya mwisho kupata pointi ilizikusanya zote tatu, ilikuwa Februari 3, 2026 ilipoichapa Mashujaa bao 1-0 ikiwa pia nyumbani.
Timu hiyo hivi sasa inafundishwa na Imani Mwalupetelo baada ya Kocha Mkuu, Abdallah Mohamed ‘Bares’ kuondoka kwa makubaliano ya pande mbili.
Rekodi zinaonesha kuwa, KMC msimu huu katika pointi tisa ilizonazo, nane imezipatia nyumbani iliposhinda mechi mbili dhidi ya Mashujaa (1-0) na ushindi kama huo mbele ya Dodoma Jiji, huku ikitoka sare dhidi ya Tanzania Prisons (1-1) na Mtibwa Sugar (0-0).
Mechi tano za nyumbani imepoteza dhidi ya Mbeya City (3-0), JKT Tanzania (1-0), Simba (2-0), Azam (2-0) na Singida Black Stars (1-0).
Ugenini KMC imecheza mechi kumi, haijashinda, imetoka sare moja dhidi ya Coastal Union (1-1), huku ikipoteza tisa dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), Fountain Gate (1-0), Yanga (4-1), Pamba Jiji (3-0), TRA United (3-0), Namungo (1-0), Dodoma Jiji (2-1), Mbeya City (3-2) na Singida Black Stars (1-0).
Kwa msimu wa 2025-2026, KMC ilianza kufundishwa na Kocha Mbrazili, Marcio Maximo aliyeiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi tisa za Ligi Kuu, kati ya hizo alishinda moja, sare moja na kuchapwa saba, huku kikosi hicho kikifunga mabao mawili na kuruhusu 14, akikiacha mkiani na pointi nne. Akaondoka Desemba 6, 2025.
Baada ya hapo, Desemba 30, Bares alitambulishwa kuiongoza KMC alipodumu hadi Aprili 3, 2026 huku akiondoka kwa kushinda mechi moja, sare moja na kupoteza sita.
KMC inayoburuza mkia na pointi tisa katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, imecheza mechi 19, imeshinda mbili sare tatu, huku ikipoteza 14, imefunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 30.