Simba SC

MAKONDA AONYA KLABU ZINAZOWEKA VIPAJI BENCHI

Vardo June 3, 2026 1:37 pm

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ametoa onyo kwa baadhi ya klabu zinazowasajili wachezaji vijana kisha kuwaweka benchi kwa muda mrefu bila kuwapa nafasi ya kucheza, akisisitiza kuwa tabia hiyo ni hatari kwa maendeleo ya vipaji na mustakabali wa soka la Tanzania.

Makonda amesema wachezaji wenye umri mdogo wanahitaji kupata muda wa kucheza mara kwa mara ili kuendelea kukua kisoka, kuongeza uzoefu na kufikia viwango vya juu.

Amesema kuwa kuwasajili vijana kwa lengo la kuwahifadhi pekee kunasababisha maendeleo yao kusimama na wakati mwingine kuua kabisa vipaji ambavyo vingekuwa tegemeo la taifa siku zijazo.

Akizungumza jijini Rabat baada ya kumalizika kwa michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, Waziri huyo alizitaka klabu zinazovutiwa na nyota hao kuhakikisha zinawapa mazingira bora ya kucheza na kuendelea kujiendeleza badala ya kuwaweka pembeni kwa muda mrefu.

Kauli hiyo imekuja baada ya Serengeti Boys kumaliza mashindano hayo katika nafasi ya pili kufuatia kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Senegal kwenye mchezo wa fainali uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 za kawaida.

“Kwa masilahi ya nchi, vijana hawa wanahitaji kucheza ili waendelee kukua na kuimarika zaidi na baadaye walitumikie taifa. Kama mnawasajili kwa kushinda halafu mnaishia kuwaweka benchi, itawasaidia nini?” alihoji Makonda

Amesema mafanikio ya muda mrefu ya soka la Tanzania hayatapatikana bila uwekezaji wa kweli katika maendeleo ya vijana, akieleza kuwa klabu zina jukumu kubwa la kuhakikisha vipaji vinapata nafasi ya kuonekana na kuendelea kuimarika kupitia ushiriki wa mara kwa mara kwenye mechi za ushindani.

Katika hatua nyingine, Makonda amemuelekeza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Oscar Mirambo kutafuta utaratibu maalumu utakaovitaka klabu zinazowasajili vijana hao kuwapa nafasi ya kucheza na kuendelea kukuza viwango vyao.

Amesema utekelezaji wa utaratibu huo utasaidia kulinda vipaji vya wachezaji vijana, kuongeza ushindani katika ligi za ndani na kuweka msingi imara wa mafanikio ya timu za taifa za Tanzania kwa miaka ijayo.

MAGORI AFICHUA MSIMAMO WA SIMBA DHIDI YA MIGOGORO YA WACHEZAJI NA MAKOCHA TWIGA STARS YAPIMA NGUVU DHIDI YA MALAWI KUELEKEA WAFCON