MAGORI AFICHUA MSIMAMO WA SIMBA DHIDI YA MIGOGORO YA WACHEZAJI NA MAKOCHA
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, ameweka wazi kuwa klabu hiyo haina deni lolote linaloweza kuifanya ikumbwe na adhabu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), akisisitiza kuwa Simba imekuwa ikitimiza wajibu wake wa kifedha kwa wakati.
Magori amesema kuwa hakuna sababu ya mashabiki wa Simba kuwa na hofu juu ya uwezekano wa klabu hiyo kufungiwa usajili au kuadhibiwa na FIFA kutokana na madai ya madeni, kwani uongozi umejipanga kuhakikisha kila anayestahili malipo yake anayapata kwa mujibu wa makubaliano.
Ameeleza kuwa hata kama kunatokea changamoto yoyote inayohusisha mchezaji au kocha, Simba imekuwa ikimaliza masuala hayo kwa njia ya maelewano na kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria na kimkataba.
“Hatuna madeni, hakuna kitu tunachokiogopa kuhusu FIFA. Hata tukimuondoa kocha au mchezaji, tunamalizana naye na tunamlipa stahiki zake,” amesema Magori.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa moja ya misingi mikubwa inayofuatwa na klabu hiyo ni kulinda taswira na heshima ya Simba ndani na nje ya nchi, jambo ambalo limekuwa likipewa kipaumbele na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (Mo Dewji).
Kwa mujibu wa Magori, Mo Dewji amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna jambo linaloweza kuichafua Simba, ikiwemo kuchelewesha au kutolipa madai halali ya waliowahi kuitumikia klabu hiyo.
Amesisitiza kuwa wakati mwingine klabu imekuwa ikitoa fedha zaidi ya kiwango kilichopo kwenye mikataba kwa lengo la kuhakikisha pande zote zinamaliza tofauti zao kwa amani na kulinda hadhi ya Simba, huku akiwataka mashabiki kuendelea kuwa na imani na uongozi uliopo