TWIGA STARS YAPIMA NGUVU DHIDI YA MALAWI KUELEKEA WAFCON
TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, leo itakuwa na kibarua kizito itakapomenyana na Malawi katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 10:00 jioni.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi kwa mataifa hayo mawili yanayojiandaa kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), huku kila upande ukitafuta kupima kiwango chake kabla ya mashindano hayo makubwa.
Kocha Msaidizi wa Twiga Stars, Edna Lema, amesema mchezo huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa utatoa taswira halisi ya hatua ya maandalizi ya timu pamoja na maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho.
Amesema ushindi dhidi ya Malawi utakuwa chachu ya kuongeza morali kwa wachezaji na kuijengea timu kujiamini zaidi kuelekea WAFCON, sambamba na kuimarisha ushindani ndani ya kikosi.
“Malawi na Tanzania zote zinaelekea WAFCON, hivyo mechi hii itatupa picha halisi ya kiwango cha maandalizi yetu na maeneo ambayo bado yanahitaji maboresho kabla ya mashindano kuanza,” amesema Edna.
Aidha, ameeleza kuwa benchi la ufundi litatumia mchezo huo kutathmini uwezo wa wachezaji mmoja mmoja pamoja na kiwango cha kikosi kwa ujumla, ili kubaini utayari wa timu katika majukumu ya kimataifa yanayokuja.
Kwa upande wa Malawi, kocha Lovemore Fazili amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri kwa mchezo huo na kinautazama kama fursa muhimu ya kujipima kabla ya WAFCON. Ameongeza kuwa wanatarajia ushindani mkali kutoka kwa Twiga Stars huku wakilenga kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa.
Kwa ujumla, mchezo huo unatarajiwa kuwa kipimo muhimu kwa timu zote mbili, ambapo makocha watapata nafasi ya kutathmini maendeleo ya vikosi vyao katika mbinu, utimamu wa mwili na uwezo wa kushindana katika ngazi ya kimataifa kuelekea WAFCON