KOCHA wa Simba SC, Steve Barker, ameweka wazi msimamo wake kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akisisitiza kuwa hataki kuona makosa madogo yakigharimu timu yake.
Kocha huyo ameonyesha umakini mkubwa kwa kila idara ya kikosi, akiamini ushindi utatokana na nidhamu, umakini na utekelezaji sahihi wa majukumu ndani ya uwanja.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani Jumapili, Aprili 19, 2026, ikiwa ugenini dhidi ya Namungo FC katika Uwanja wa Majaliwa, uliopo Ruangwa, mkoani Lindi.
Barker amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu kiwango cha wachezaji wake mazoezini, huku akibaini maeneo yanayohitaji maboresho, hususan katika safu ya ulinzi na ushambuliaji.
Ameeleza kuwa licha ya timu kuonyesha ushindani mzuri katika mechi zilizopita, bado kuna nafasi kubwa ya kuboresha ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika kila mchezo.
Katika kuonyesha uzito wa pambano hilo, tayari ameanza kupanga kikosi chake cha kwanza kwa kuzingatia ubora na mbinu za wapinzani wao.
“Hatuidharau timu yoyote, kwa sababu soka la Tanzania limekuwa na ushindani mkubwa na matokeo yanaweza kubadilika muda wowote,” amesema Barker.
Kwa upande wa wachezaji, amesema morali ipo juu, huku kila mmoja akipambana kuwania nafasi katika kikosi cha kwanza.
“Baadhi yao wako katika kiwango kizuri, jambo linalonipa kazi ngumu kuchagua nani aanze na nani asubiri benchi,” ameongeza.
Aidha, mashabiki wa Simba wameendelea kuonyesha matumaini makubwa kuelekea mchezo huo, wakiamini timu yao ina uwezo wa kufanya vizuri na kuendeleza presha katika mbio za ubingwa. Hamasa imekuwa kubwa mitandaoni na hata katika mazoezi ya timu.
Barker amesisitiza kuwa presha hiyo haitawaathiri, kwani kikosi kimejipanga kisaikolojia na kimwili kukabiliana na changamoto yoyote.