MENEJA wa Simba, Patrick Rweyemamu, amefunguka kuhusu hali ya beki Nickson Kibabage, akieleza kuwa mchezaji huyo anaendelea vizuri kiafya na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Muungano.
Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka kati ya Jumanne au Jumatano kwenda visiwani humo, kikiwa na lengo la kushiriki mashindano hayo ambayo yamekuwa na ushindani mkubwa kila mwaka.
Rweyemamu amebainisha kuwa mipango yao ni kusafiri na kikosi kizima, akiwemo Kibabage ambaye alikosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Namungo FC kutokana na majeraha madogo pamoja na kupewa mapumziko baada ya kucheza mechi nyingi mfululizo.
Amesema kurejea kwa Kibabage kutategemea tathmini ya mwisho kutoka kwa daktari wa timu, lakini kwa sasa hali yake inaonesha kuimarika na ana nafasi kubwa ya kuwa sehemu ya kikosi kitakachoenda Zanzibar.
“Tumerejea Dar es Salaam salama na sasa tunajiandaa na safari ya kwenda Zanzibar kwa ajili ya mashindano ya Muungano. Kwetu sisi, huu ni ushindani muhimu, hivyo tunaenda kupambana tukiwa na kikosi chetu kamili,” amesema Rweyemamu.
“Kibabage atakuwa sehemu ya wachezaji watakaosafiri. Alikuwa na majeraha madogo na pia alipumzishwa kutokana na mzigo wa mechi nyingi. Daktari wa timu ataendelea kumfuatilia kabla ya safari,” ameongeza.
Katika mashindano hayo, Simba wanatarajiwa kushuka dimbani Alhamisi, Aprili 23, ambapo wataikaribisha Mafunzo SC katika Uwanja wa New Amaan Complex, mchezo utakaochezwa majira ya saa 2:15 usiku.