BABU FERGUSON AONEKANA HADHARANI
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, mwenye umri wa miaka 84, ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu alipopelekwa hospitalini mwezi Machi kutokana na kuugua ghafla.
Ferguson ambaye ni mmoja kati ya makocha wakubwa zaidi duniani alionekana kwenye mgahawa mmoja mjini Wilmslow, akiwa na shabiki mmoja wa Manchester United, akionyesha tabasamu huku akiwa mwenye afya njema.
Haya ni mabadiliko chanya ikizingatiwa kuwa Machi aliugua akiwa katika Uwanja wa Old Trafford kabla ya Manchester United kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya Liverpool, kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, ‘Premier’.
Tukio hilo lilikuwa tahadhari tu kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani kupumzika, lakini juzi alionekana mwenye afya njema na akitembea bila msaada wowote.
Fergie amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England mara 13 akiwa kocha mwenye mafanikio makubwa zaidi kwenye timu hiyo na ligi kwa ujumla.
Shabiki aliyekutana naye, Vimal Devassy, alieleza hisia zake kwenye mtandao wa Instagram:
“Si kila picha inaeleza hadithi, baadhi zinabeba hisia. Sihisi kutetemeka kwa sababu nilikutana na kiongozi wa soka, bali nilitetemeka kwa sababu nilikuwa karibu na mtu aliyechangia safari ya ushabiki wangu kwa Cristiano Ronaldo. Sihitaji kuwa shabiki mkubwa wa Manchester United, lakini heshima yangu kwa Sir Alex Ferguson na uhusiano wake wa kipekee na Ronaldo kimekuwa chanzo cha msukumo wangu. Ni tukio ambalo sitalisahau. Asante, Sir Alex.”
Devassy pia aliwaambia waandishi wa Sun Sport:
“Nilimkutana naye kwenye mgahawa wetu, na kabla hajatoka, niliomba tupige picha pamoja. Alikubali kwa furaha, jambo ambalo nililithamini sana. Ilikuwa tukio dogo lakini maalumu ambalo nitakumbuka daima.”
Sir Alex, meneja mwenye mafanikio makubwa katika historia ya Manchester United, ni mmoja wa mashabiki wa kawaida wa mechi za nyumbani na ugenini za United. Alihudhuria Old Trafford kabla ya mechi kubwa ya Ligi Kuu kati ya United na watani wa Liverpool. Hata hivyo, ingawa alikua na nafasi ya kuwa balozi wa klabu na kupata ruhusa ya kuingia vyumba vya wachezaji wa kikosi cha kwanza, baadhi ya haki hizo zimepunguzwa chini ya uongozi wa Sir Jim Ratcliffe na sasa anabaki kuwa shabaki wa kawaida kabisa jukwaani.
Historia ya ugonjwa inaonyesha kuwa Ferguson alipata ugonjwa wa kuvuja damu kichwani mwaka 2018, lakini akapona baada ya upasuaji. Hakuna dalili kwamba tukio hili la Machi liligusa hali hiyo ya awali bali inaelezwa kuwa alikuwa mchovu kutokana na pilika nyingi za bila kupumzika.
Tangu alipostaafu uongozi wa Manchester United mwaka 2013, Ferguson amekabili changamoto nyingi za kiafya. Mwaka 2018 alipata upasuaji wa dharura kichwani, ambapo madaktari walimpa uwezekano wa 20% kuishi lakini Mungu alimsaidia na anaendelea kupambana hadi leo. Katika filamu yake aliyotoa mwaka 2021, “Sir Alex Ferguson: Never Give In”, ameeleza:
“Kulikuwa na kuvuja damu kichwani mara tano siku hiyo. Watu watatu tuliokuwa hosipitali moja walikufa, wawili tukaendelea kuishi. Hii ni bahati.”
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Fergie alianza kuwa na huzuni na maradhi ya mara kwa mara baada ya kumpoteza mke wake Cathy mwaka 2023, ambaye walikuwa wamekaa kwenye ndoa kwa miaka 57. Lady Cathy alifariki akiwa na umri wa miaka 84 na ndiye alikuwa rafiki mkubwa wa kocha huyo raia wa Scotland.
MAFANIKIO AKIWA MAN UNITED
Premier League-13
Kombe la FA- 05
Kombe la Ligi- 04
Ngao-10
UEFA- 02
Klabu Bingwa Dunia-01