MSAKO WA POINTI TATU TANZANIA PRISONS
TANZANIA Prisons inaendelea kujifua kwa ajili ya mechi tano zilizobaki, huku kocha mkuu wa timu hiyo Shedrack Nsajigwa akitangaza msako mpya wa pointi tatu kila mchezo ili kuihakikishia timu hiyo kukwepa kushuka daraja.
Prisons haipo sehemu nzuri ikiwa nafasi ya pili kutoka mkiani na pointi 20, ambapo Juni 14 itakuwa nyumbani kuwakaribisha Dodoma Jiji kabla ya kuwafuata JKT Tanzania, Singida Black Stars kisha kurudi nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar na kuhitimishia ugenini kwa Mashujaa FC.
Kwa sasa ligi hiyo imesimama kupisha mechi za kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambapo Tanzania Prisons inaendelea na mazoezi kujiwinda na mechi zilizobaki huku wachezaji wakionesha ari na morali kikosini haswa baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Pamba Jiji.
Akizungumza na Soka la Bongo Nsajigwa amesema kwa sasa hawana hesabu zozote zaidi ya pointi tatu kila mchezo kutokana na matokeo waliyonayo hivi sasa na kwamba matarajio yake ni kufanya vizuri.
Amesema licha ya hatari waliyopo kwenye msimamo, lakini lolote linaweza kutokea kwakuwa uwezo na uzoefu walionao timu kwenye ligi hiyo na sapoti ya mashabiki na uongozi watafikia malengo.
“Ndio maana tumeendelea na mazoezi kusahihisha makosa na kuboresha tulipofanikiwa, kimsingi hatuna mchezo mmoja bali zote zilizobaki tunahitaji ushindi, tunajua presha iliyopo ila tumejipanga”
“Lazima tujiandae kiakili, kisaikolojia na kiufundi kuhakikisha kila mchezo bila kujali nyumbani au ugenini, bado tunayo nafasi ya kuipambania timu kwakuwa ligi haijaisha” amesema Nsajigwa.
Kocha huyo amewapongeza nyota wake kwa namna wanavyojituma akieleza kuwa kwa sasa akili na nguvu zao zinawafikiria zaidi mchezo ujao dhidi ya Dodoma Jiji kuhakikisha wanashinda na kujiondoa nafasi za chini.
Huu ni msimu wa pili Prisons inakuwa kwenye hali mbaya baada msimu uliopita kuponea chupuchuopu kushuka daraja.