KOCHA SERENGETI BOYS AOMBA MANNE
BAADA ya kuipeleka Tanzania kwenye Fainali za Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika nchini Qatar, Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu, amesema kazi kubwa iliyobaki sasa ni kuhakikisha timu hiyo inapata maandalizi ya kiwango cha kutosha ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.
Tanzania ilifuzu kucheza Kombe la Dunia baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika kwa vijana, ikimaliza nafasi ya pili baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-2 na Senegal kufuatia sare ya 1-1 dakika tisini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nsanganzelu amesema tayari timu hiyo imefuzu na huo ni mwanzo wa jukumu kubwa zaidi la kuandaa kikosi kitakachokwenda kushindana na mataifa bora duniani.
Amesema ili Serengeti Boys iweze kushindana na vigogo wa soka la dunia, ni lazima ipewe maandalizi ya kutosha yanayojumuisha mechi nyingi za kirafiki dhidi ya timu kutoka mataifa yaliyoendelea kisoka.
“Kombe la Dunia ni kiwango tofauti kabisa. Tunahitaji mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya timu bora ili vijana wetu wajifunze kasi ya mchezo, ushindani na mazingira ya mashindano makubwa kabla ya kwenda Qatar,” amesema Nsanganzelu.
Kocha huyo amesema mafanikio ya timu hayatategemea benchi la ufundi pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa wadau wote wa soka kuanzia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Serikali na wadhamini mbalimbali.
Nsanganzelu aliomba mambo manne ambayo ni lishe bora kwa wachezaji, huduma za kitabibu za kisasa, vifaa vya mazoezi pamoja na mazingira mazuri ya kambi.
“Vijana hawa wameonyesha wana uwezo mkubwa. Kilichobaki ni kuwapa mazingira bora ya kujiandaa. Lishe bora, huduma za afya, vifaa vya kisasa na mechi za ushindani ni vitu vinavyoweza kutusaidia kufika mbali zaidi,” amesema.
Aliongeza kuwa tofauti kubwa kati ya mataifa yanayotawala soka la vijana duniani na Tanzania si vipaji, bali ni uwekezaji wa kisayansi katika maendeleo ya wachezaji tangu wakiwa wadogo.
“Waandishi mtusaidie kupaza sauti. Sio kwamba vipaji hatuna, tunavyo, ila tunahitaji mfumo bora wa kuwaendeleza vijana, kuwajengea uwezo wa kimwili, kiufundi na kiakili. Tukifanya hivyo tutakuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri Qatar,” amesema.
Takribani timu 48 zilizofuzu kucheza Kombe la Dunia zitashindana nchini Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13 kuwania ubingwa wa michuano hiyo.
Tanzania iliyofuzu kupitia mashindano ya AFCON imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Jamhuri ya Ireland na Costa Rica.