Yanga SC

YANGA YAJIAMINI, HERSI ASEMA SAFARI YA UBINGWA MSIMU HUU NI NYEPESI

Vardo June 5, 2026 3:11 pm

RAIS wa Yanga SC, Eng. Hersi Said, ametoa kauli yenye kuonesha kujiamini kubwa kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akisema kuwa timu yake ina nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake kuliko ilivyokuwa msimu uliopita.

Hersi amesema msimu uliopita ulikuwa wa changamoto kubwa kwa mabingwa hao, huku ushindani ukiwa mkali hadi hatua za mwisho kabisa za ligi.

Amefafanua kuwa iliwalazimu kusubiri hadi mechi ya mwisho ya msimu ndipo wapate uhakika wa kutwaa ubingwa, hali iliyofanya presha ya mashindano kuwa kubwa zaidi kuliko kawaida.

Hersi amebainisha kuwa moja ya vipindi vigumu zaidi ilikuwa ni mchezo wa Dabi ya Dar es Salaam dhidi ya Simba SC, ambao ulihitimisha msimu na kuwa na mchango mkubwa katika safari ya ubingwa wao.

“Nadhani msimu uliopita ndio ulikuwa msimu mgumu sana kwetu kwa sababu tulilazimika kushinda mechi yetu ya mwisho, tena Dabi dhidi ya Simba SC, ili tuwe mabingwa,” amesema.

 

Ameongeza kuwa kwa sasa hali ni tofauti, akiamini kikosi kimeimarika zaidi na kina uwezo wa kushinda ligi bila kupata presha kubwa kama ya msimu uliopita.

“Sioni kama ubingwa wa msimu huu ni mgumu kama ilivyokuwa msimu uliopita,” ameongeza, kauli inayoonesha matumaini makubwa ndani ya uongozi wa Yanga kuelekea safari mpya ya ligi.

YANGA YAWEKA KAMBI SOKONI, WAKABAJI KIPAUMBELE KIKUBWA KOCHA SERENGETI BOYS AOMBA MANNE