Yanga SC

YANGA YAWEKA KAMBI SOKONI, WAKABAJI KIPAUMBELE KIKUBWA

Vardo June 5, 2026 2:59 pm

KLABU ya Yanga imeendelea kuathiriwa na pengo lililoachwa na kiungo mkabaji Khalid Aucho baada ya kuondoka na kujiunga na Singida Black Stars, huku uongozi wa timu hiyo ukiingia sokoni kusaka wachezaji wa kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa tangu Aucho aondoke, Yanga imekuwa ikitafuta mchezaji mwenye uwezo wa kuziba nafasi yake, lakini hadi sasa bado haijampata kiungo anayekidhi viwango na majukumu aliyokuwa akiyatekeleza nyota huyo wa Uganda.

 

Kutokana na hali hiyo, mabingwa hao watetezi wameanza rasmi mchakato wa kutafuta wachezaji watatu muhimu watakaoongeza ushindani ndani ya kikosi na kusaidia kufanikisha malengo ya msimu ujao wa mashindano ya ndani na kimataifa.

 

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Yanga inahitaji kusajili beki mmoja wa kati mzawa pamoja na viungo wawili wakabaji watakaokuwa na uwezo wa kuimarisha eneo la kiungo cha ulinzi ambalo limeonekana kuwa na changamoto tangu kuondoka kwa Aucho.

“Tunatafuta beki mmoja wa kati mzawa ambaye atakuja kuongeza ushindani na kushirikiana vizuri na Ibrahim Bacca.

Kuhusu Job Dickson tunaamini atakuwa amepona kikamilifu, lakini bado tunaangalia uwezekano wa kuongeza nguvu katika eneo hilo,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa iwapo watampata beki bora zaidi wa ndani, kuna uwezekano wa kumruhusu Frank Asisiki kuondoka ili kufungua nafasi kwa maboresho mengine ndani ya kikosi.

 

Msimu uliopita Yanga ilionyesha ubora mkubwa katika mashindano ya ndani, lakini pengo la Aucho limeendelea kuonekana katika baadhi ya michezo.

 

Hivyo, usajili wa viungo wapya unaonekana kuwa moja ya vipaumbele vikubwa vya klabu hiyo katika maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

KASSALI AWEKA PRESHA, CAMARA ASUBIRI HATIMA YAKE SIMBA YANGA YAJIAMINI, HERSI ASEMA SAFARI YA UBINGWA MSIMU HUU NI NYEPESI