KASSALI AWEKA PRESHA, CAMARA ASUBIRI HATIMA YAKE SIMBA
HATMA ya kipa wa Simba, Moussa Camara, kuendelea kusalia ndani ya kikosi hicho baada ya msimu huu bado haijajulikana, huku uamuzi wa mwisho ukisubiriwa kutoka kwa benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Steve Barker.
Camara ameshindwa kuitumikia Simba kwa sehemu kubwa ya msimu huu kutokana na majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu, hali iliyomfanya kupoteza nafasi yake kikosini
Katika kipindi hicho, nafasi yake ilizibwa na kipa raia wa Guinea, Djibril Kassali, ambaye ameendelea kuwa chaguo la kwanza langoni mwa Wekundu wa Msimbazi.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema uongozi wa klabu ulilazimika kufanya maamuzi ya haraka baada ya Camara kushindwa kupona kwa wakati huku timu ikiwa inakabiliwa na mashindano muhimu.
Magori ameeleza kuwa wakati huo Simba ilikuwa imebaki na kipa mmoja mwenye uzoefu, Abel Hussein, huku Camara na Yakubu Suleiman wakiwa majeruhi na wakihitaji muda mrefu kurejea uwanjani.
“Tuliamua kuingia sokoni kutafuta kipa mwingine na hapo ndipo tukampata Djibril Kassali. Camara mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo uamuzi wa kama atapewa mkataba mpya au la utatolewa na benchi la ufundi,” amesema Magori.
Ameongeza kuwa iwapo benchi la ufundi litashauri Camara aongezewe mkataba, uongozi uko tayari kutekeleza ushauri huo. Hata hivyo, kama litachagua kuendelea na Kassali au kufanya maamuzi mengine, klabu itafuata mwelekeo huo.
“Kanuni zetu zinahitaji timu kuwa na kipa mmoja wa kigeni, hivyo tutakaa na kuamua nini kifanyike baada ya kupokea mapendekezo ya benchi la ufundi,” amesisitiza Magori.