KAIZA CHIEFS WAVAMIA MSIMBAZI KWA KIUNGO
UONGOZI wa Simba umejikuta katika vita ya usajili na klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, baada ya timu hiyo kuonyesha nia ya kutaka kumnasa kiungo mshambuliaji Neo Maema kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Maema kwa sasa anakipiga ndani ya Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Mamelodi Sundowns, ambapo amekuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho katika kampeni za mashindano ya ndani na kimataifa.
Mkataba wake wa mkopo unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia macho ya klabu mbalimbali.
Licha ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa Msimbazi, bado Simba haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wa nyota huyo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa viongozi wanaendelea kutathmini hali ya kikosi kabla ya kutoa msimamo rasmi juu ya uwezekano wa kumbakisha Maema kwa msimu mwingine.
Inaelezwa kuwa hatma ya mchezaji huyo ipo mikononi mwa benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu Steve Barker, ambaye anatarajiwa kufanya tathmini ya kina ya kikosi chake mara baada ya kumalizika kwa msimu huu kabla ya kupendekeza maeneo ya kuimarishwa.
Wakati Simba ikisubiri maamuzi ya kiufundi, Kaizer Chiefs imeanza kuonyesha hatua za awali za kutaka kumrejesha Maema nchini kwao.
Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa klabu hiyo tayari wamewasiliana na wawakilishi wa mchezaji huyo ili kufahamu masharti na uwezekano wa kufanikisha usajili huo.
Hata hivyo, mazungumzo hayo bado yapo katika hatua za mwanzo, huku kukiwa hakuna makubaliano yoyote rasmi yaliyofikiwa kati ya pande husika.
Chanzo kimoja kilieleza kuwa hatua kubwa zaidi zinatarajiwa kuchukuliwa mara baada ya msimu kumalizika.
Kwa sasa, mustakabali wa Neo Maema unaendelea kubaki kitendawili, huku Simba na Kaizer Chiefs zikitajwa kuwa kwenye mbio za kuwania saini yake. Mashabiki wa soka nchini Tanzania na Afrika Kusini wameendelea kusubiri kwa hamu kuona ni wapi kiungo huyo atacheza msimu ujao.