UONGOZI wa TRA United umeibuka na kuweka mambo hadharani kufuatia taarifa zilizoenea zikimhusisha nyota wao, Ramadhan Salum maarufu kama ‘Chobwedo’, na tetesi za kusaini mkataba na vigogo wa soka nchini, Simba SC au Young Africans SC.
Kupitia Mwenyekiti wa klabu hiyo, Kamna Shomari, uongozi huo umevunja ukimya na kusisitiza kuwa hadi sasa hakuna taarifa rasmi yoyote inayothibitisha kuondoka kwa kiungo huyo.
Amesema mchezaji huyo bado ana mkataba halali na anaendelea kuitumikia timu hiyo kama kawaida.
Kamna ameweka wazi kuwa klabu hiyo inafuata taratibu za kisheria katika masuala ya usajili, akisisitiza kuwa hakuna klabu yoyote iliyowasiliana nao rasmi kuhitaji huduma ya Chobwedo.
Ameongeza kuwa ikiwa kuna timu inahitaji kumsajili, ni lazima ifuate njia sahihi za mawasiliano na uongozi wa TRA United.
“Hatuna taarifa zozote za Chobwedo kusaini timu nyingine. Bado yupo nasi na anaendelea na majukumu yake. Sisi tunaheshimu taratibu, hivyo klabu yoyote inayomhitaji inapaswa kuwasiliana nasi moja kwa moja,” amesema Kamna.
Katika kipindi hiki cha msimu, Chobwedo amekuwa mmoja wa wachezaji waliovutia macho ya mashabiki na wadau wa soka, hasa kutokana na kiwango chake bora anachoonyesha uwanjani.
Uwezo wake huo umeonekana kuwa kichocheo cha tetesi za kuwindwa na klabu kubwa, huku zikielezwa mipango ya kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao.
Hata hivyo, pamoja na mvuto huo, hatma ya nyota huyo bado ipo mikononi mwa TRA United, ambao wanaonekana kutokuwa tayari kumuachia kirahisi bila kufuata taratibu zote zinazohitajika kisheria na kimkataba.