KOCHA wa Simba, Steve Barker, amesisitiza umuhimu wa wachezaji wake kuwa tayari muda wote wanapoitumikia timu hiyo, akieleza kuwa kila mmoja anapaswa kupambania nembo ya klabu kwa kujituma na nidhamu ya hali ya juu.
Simba inatarajia kusafiri kuelekea Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Muungano, itakayofanyika kuanzia Jumanne, Aprili 21 hadi 29, 2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex. Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na ushindani mkali huku timu mbalimbali zikisaka ubingwa.
Barker amesema maandalizi ya kikosi chake yako katika hali nzuri, akibainisha kuwa morali ya wachezaji ipo juu na kila mmoja ana hamasa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo muhimu.
Kocha huyo pia alieleza kufurahishwa na kurejea kwa nyota wake wawili, Shomari Kapombe na Yusuph Kagoma, ambao walikosekana katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo FC, ambapo Simba iliibuka na ushindi.
Aliongeza kuwa kurejea kwa wachezaji hao kunaongeza nguvu ndani ya kikosi chake na kumpa chaguo pana zaidi katika kupanga kikosi kitakachoshiriki mashindano hayo.
“Kila mchezaji ana nafasi ya kupambania nembo ya klabu, hivyo ni lazima awe tayari muda wote. Morali ya kikosi ipo vizuri na tunaenda kushindana kwa malengo ya kufanya vizuri,” amesema Barker.
Simba inaingia kwenye michuano hiyo ikiwa na matarajio makubwa ya kufanya vyema, huku benchi la ufundi likiamini kuwa maandalizi waliyonayo yatawasaidia kufikia malengo yao.