Home Habari za michezo
0

MANCHESTER, ENGLAND: INGAWA Erling Haaland ndiye aliyefunga bao la ushindi katika ushindi wa mabao 2-1 wa Manchester City dhidi ya Arsenal, Jumapili iliyopita, sasa ameamua kumtaja mchezaji bora wa mechi hiyo akisema nahodha wake, Bernardo Silva, alistahili kubeba tuzo baada ya mchezo kumalizika na kilichofanyika kumpa ilikuwa sahihi.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno anatarajiwa kuondoka Man City baada ya misimu tisa yenye mafanikio makubwa, na kiwango chake dhidi ya Arsenal kilikumbushia juu ya kile ambacho kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kitapoteza.

Haaland alikuwa akimaanisha tukio muhimu ambapo Bernardo alizuia hatari kwa kupiga mpira wa kichwa ndani ya eneo lake la hatari, akimzidi nguvu straika wa Man City, Viktor Gyokeres licha ya tofauti ya kimo. Ingawa wanacheza nafasi tofauti kulinganisha na Fabio Cannavaro, bingwa wa Kombe la Dunia na mshindi wa Ballon d’Or 2006, lakini Bernardo anafananishwa kucheza kama mkongwe huyo.

Kama Cannavaro, Bernardo siyo mrefu wala mwenye nguvu nyingi kimwili, lakini hufanya uamuzi wake kwa muda sahihi, ujasiri na uwezo wa kusoma mchezo. Kulikuwa pia na tukio jingine alipomkimbiza Kai Havertz na kuzuia hatari licha ya kuwa mpinzani wake alikuwa na nguvu zaidi.

Ramani ya mguso wake wa mpira inaonyesha jinsi alivyojihusisha kila sehemu ya uwanja, akiwa na mchango mkubwa hata katika eneo la ulinzi. Bila mpira, alifanya kazi kubwa akifanikiwa kufunika eneo la umbali wa kilomita 12.3 zaidi ya mchezaji yeyote uwanjani. Hii inaendana na msimu wake kwa ujumla, ambapo amekimbia umbali mkubwa zaidi kuliko mchezaji yeyote wa Ma City katika Ligi Kuu England (kilomita 327).

Akiwa na mpira, pamoja na Rodri, alisimamia mchezo na kuunganisha pasi hasa kipindi cha pili ambapo Man City walitawala. Ushirikiano wa pasi kati ya Bernardo na Rodri ulikuwa wa juu zaidi, huku Man City wakiongeza mashambulizi yao kuingia katika eneo la mwisho kutoka mara 11 hadi 33, na miguso ndani ya boksi la Arsenal kutoka 15 hadi 25.

Huo ulikuwa mfano mwingine wa mchezaji anayeaminika sana na Guardiola kuonyesha ubora wake katika mechi kubwa. Kwa ushindi huo, Bernardo alifikia rekodi ya David Silva ya ushindi mwingi katika Ligi Kuu England akiwa na Man City.

Guardiola mwenyewe alionekana kuguswa sana alipomzungumzia mchezaji huyo, akisema: “Ukiendelea kuzungumzia kuhusu yeye, nitalia.  Itakuwa ngumu sana siku atakapoondoka. Bernardo ni Bernardo huwezi kumuelezea. Bila yeye, miaka yangu tisa hapa ingekuwa tofauti kabisa. Ni mchezaji wa kipekee.”

Tangu ajiunge na klabu hiyo 2017/18, Bernardo hajawahi kucheza chini ya mechi 45 kwa msimu, akicheza 452 katika mashindano yote ikiwa ni zaidi ya mchezaji yeyote katika ligi tano bora Ulaya akiwazidi Mohamed Salah (439) na Antoine Griezmann (434). Man City tayari wamewaaga wachezaji muhimu kama Kevin De Bruyne, İlkay Gundogan, Fernandinho na David Silva.

Kwa sasa, wachezaji wachache waliobaki wenye uzoefu wa kushinda mara kwa mara ni pamoja na Rodri na Bernardo. Ikiwa Rodri anakuwa na majeraha, Bernardo anaweza kubeba jukumu la uongozi tena mwishoni mwa msimu na kubeba taji la saba la Ligi Kuu England.