Home Habari za michezo DALILI NJEMA, YANGA WAANZA KUSHTUKA

DALILI NJEMA, YANGA WAANZA KUSHTUKA

0

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steven Barker, amevunja ukimya kuhusu mchakato wa kuiunganisha timu yake mpya, akieleza wazi kuwa safari hiyo haikuwa rahisi kama wengi walivyodhani.

Barker amesema changamoto kubwa iliyowakabili ilikuwa ni muda mfupi wa maandalizi, hali iliyowalazimu kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha wachezaji wapya wanaendana haraka na mfumo wake wa uchezaji.

Hata hivyo, kocha huyo ameweka bayana kuwa juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda. Kupitia mazoezi ya pamoja na mbinu maalum walizozitumia, kikosi hicho sasa kinaonyesha dalili nzuri za muunganiko imara.

Ameongeza kuwa viashiria vya ubora vinaendelea kuonekana kadri siku zinavyosonga mbele, jambo linaloleta matumaini makubwa kwa mashabiki pamoja na uongozi wa klabu hiyo.

“Haikuwa rahisi kuunganisha wachezaji wengi wapya bila maandalizi ya muda mrefu, lakini kwa kufanya kazi kwa karibu na wachezaji, tumepata muunganiko na naamini kuna mengi mazuri yanakuja,” amesema Barker.

Amefafanua kuwa anajenga timu yenye uwiano mzuri kati ya ulinzi, viungo na ushambuliaji, akisisitiza kuwa mafanikio ya timu yoyote yanatokana na kuwa imara nyuma na kuwa na makali mbele.

Kwa mujibu wa Barker, kila kipindi cha mazoezi kinalenga kuboresha safu zote kwa pamoja ili kuepuka kuegemea upande mmoja, huku akisisitiza kuwa bado hawajafika wanapotaka kufika.

“Ni safari ndefu, lakini kinachonipa faraja ni nidhamu na kujituma kwa wachezaji wangu. Kila siku tunaendelea kuboresha na kufanyia kazi mapungufu yaliyopo,” ameongeza.

Kocha huyo amehitimisha kwa kusisitiza kuwa dhamira yake kuu ni kuirejesha Simba kwenye ubora wake wa juu, ili iwe tishio ndani na nje ya nchi, huku lengo kubwa likiwa ni kuwapa mashabiki furaha wanayoistahili kupitia matokeo mazuri uwanjani.