Home Habari za michezo DONGO ZITO, SIMBA WAIWASHA YANGA SC

DONGO ZITO, SIMBA WAIWASHA YANGA SC

0

MENEJA a Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameanza kuwarushia vijembe watani wao wa jadi, Yanga, akisisitiza kuwa kikosi chao hakina presha yoyote—hasa katika nafasi ya beki wa kushoto kwa miaka kadhaa ijayo.

Kauli hiyo imekuja kufuatia kiwango bora kinachoonyeshwa na mabeki wa kushoto wa Simba, Nickson Kibabage na Antony Mligo, ambao wamekuwa nguzo muhimu ndani ya kikosi kinachonolewa na Kocha Mkuu, Steven Barker.

Wawili hao wameonyesha uthabiti mkubwa uwanjani, jambo linaloifanya Simba kujivunia uimara wa safu hiyo. Hali hii imeonekana kuwagusa moja kwa moja watani zao wa Jangwani, ambao kwa misimu kadhaa wamekuwa wakihaha kusaka suluhisho la kudumu katika nafasi hiyo.

Inaelezwa kuwa Yanga bado wako kwenye harakati za kutafuta beki wa kushoto, huku tetesi zikidai kuwa wameonyesha nia ya kumchunguza Valentino Nouma wa TRA United ili kuimarisha eneo hilo.

Nouma alitewahi kupita Simba kabla ya kumuacha na kwenda kucheza TRA United kwa msimu huu.

Akizungumzia hali ya kikosi chake, Ahmed Ally ameweka wazi kuwa Simba ipo salama kabisa upande huo, akibainisha kuwa hata mmoja kati ya Kibabage au Mligo anapokosekana, pengo halionekani kutokana na ubora wao.

Ameongeza kuwa benchi la ufundi lina imani kubwa na mabeki hao, hali inayompa utulivu kocha Barker kupanga kikosi chake bila wasiwasi wowote upande wa ulinzi wa kushoto.

“Upande wetu wa kushoto upo salama kwa miaka 10 ijayo, Inshallah. Kibabage na Mligo ni juu moto chini moto, wana umri sahihi wa mpira na ni vipaji halisi,” amesema  Ahmed.

Kwa mtazamo huo, Simba haina mpango wa kuingia sokoni kusaka beki wa kushoto katika dirisha lijalo, ikiamini kuwa rasilimali iliyopo inatosha kabisa kukidhi mahitaji ya timu.

Wakati huohuo, kauli ya Ahmed imezidi kupandisha presha kuelekea Kariakoo Derby inayosubiriwa kwa hamu kubwa, ambapo Simba watakuwa wenyeji wa pambano hilo la watani wa jadi.