Home Habari za michezo SIMBA KWENYE HATARI, MAFUNZO SC WAJIPANGA KUWASTUA MAPEMA

SIMBA KWENYE HATARI, MAFUNZO SC WAJIPANGA KUWASTUA MAPEMA

0

KOCHA wa Mafunzo SC, Haji Mwambwe, ameweka wazi dhamira ya timu yake kuelekea michuano ya Kombe la Muungano, akisisitiza kuwa lengo lao ni kuandika historia mpya kupitia ushindani mkubwa watakaoukutana nao.

Mwambwe amesema kikosi chake kimejiandaa kikamilifu, kikiwa na ari na morali ya juu ya kupambana dhidi ya wapinzani wao, akiwemo Simba.

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Mwambwe alieleza kuwa wamefanya kazi kubwa kuhakikisha wanakuwa tayari kiakili na kimwili kwa ajili ya changamoto hiyo.

Amesisitiza kuwa licha ya ukubwa wa wapinzani wao, Mafunzo SC haitashuka dimbani kwa hofu bali kwa kujiamini na kupambana kusaka matokeo chanya.

“Mchezo dhidi ya Simba ni nafasi muhimu kwa wachezaji wetu vijana kuonyesha uwezo wao, hii ni fursa adhimu kwetu  kujitangaza na kuvutia macho ya timu kubwa,  wanapaswa  kutumia vizuri dakika watakazopata uwanjani,” amesema kocha huyo.

Kuhusu mbinu watakazotumia, Mwambwe amesema  wana faida ya kuwafahamu vizuri wapinzani wao. kuwa kila mchezaji anatambua majukumu yake na namna ya kukabiliana na changamoto atakayokutana nayo uwanjani, jambo ambalo linaongeza matumaini ya kufanya vizuri.

“Tunakutana na timu ambayo huenda haitufahamu sana, lakini sisi tunawafahamu vizuri. Hilo linatupa nafasi ya kupanga mikakati sahihi ya kuwazuia na kuwashambulia kwa ufanisi,” amesema  Mwambwe.

Kocha huyo amegusia  suala la presha kwa wachezaji wake, kuwa tayari ameondoa hofu ndani ya kikosi hicho na  wamejengewa moyo wa ushindani na hawapaswi kuwaogopa wapinzani wakubwa, bali wanatakiwa kucheza kwa uhuru na kuonyesha uwezo wao.

Mafunzo SC wanatarajiwa kushuka dimbani kesho Aprili 23 katika mchezo wao wa kwanza wa michuano hiyo, wakiwa na dhamira ya kuanza vyema safari yao ya kutafuta mafanikio na kuandika historia mpya ndani ya mashindano ya Kombe la Muungano.