UONGOZI wa klabu ya Yanga unakabiliwa na wakati mgumu katika juhudi za kuwashawishi baadhi ya nyota wake kusalia ndani ya kikosi hicho kuelekea msimu ujao.
Timu hiyo inaingia katika kipindi nyeti cha kuhakikisha inaendelea kuwa na kikosi imara, kufuatia taarifa zinazoeleza kuwa baadhi ya wachezaji wake muhimu wanawindwa na vilabu vya nje ya Tanzania.
Hali hiyo imeanza kuzua mjadala miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka kuhusu hatima ya kikosi hicho msimu ujao.
Inaelezwa kuwa kipa tegemeo wa timu hiyo, Djigui Diarra, yupo kwenye rada za klabu ya Espérance Sportive de Tunis, jambo linaloweza kuwa pigo kubwa kwa safu ya ulinzi ya Yanga endapo ataondoka.
Diarra amekuwa mhimili muhimu kutokana na kiwango chake bora langoni, hali inayomfanya aongoze miongoni mwa makipa bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa zinaeleza kuwa kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua anahusishwa na kuhitajika na JS Kabylie, huku beki Ibrahim Bacca akitajwa kuwindwa na Raja Casablanca.
“Yanga inaweza kupoteza sehemu kubwa ya uti wa mgongo wa kikosi chake. Kazi kubwa iliyopo ni kuhakikisha wanawabakisha nyota hao huku wakiendelea kuimarisha kikosi kupitia usajili wa nafasi zenye mapungufu,” amesema chanzo hicho.
Shinikizo linaendelea kuongezeka kwa uongozi wa Yanga kuhakikisha unawabakisha wachezaji hao muhimu, au kuanza mapema mchakato wa kutafuta mbadala wenye ubora sawa au zaidi.
Maamuzi yatakayochukuliwa katika kipindi hiki yanatajwa kuwa na athari kubwa kwa ushindani wa timu hiyo katika michuano ya ndani na kimataifa.