Home Habari za michezo SIMBA WAITAKA YANGA ZANZIBAR NA BARA

SIMBA WAITAKA YANGA ZANZIBAR NA BARA

0

UONGOZI a klabu ya Simba umeweka wazi dhamira yao kubwa kuelekea michuano ya Kombe la Muungano,  Visiwani Zanzibar, wakisisitiza lengo lao si kutwaa ubingwa pekee, bali pia kutumia mashindano hayo kama maandalizi muhimu kuelekea Kariakoo Derby dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Yanga, iwe Zanzibar au Bara.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka leo mchana kuelekea Zanzibar tayari kwa kushiriki michuano hiyo itakayowakutanisha na timu mbalimbali.

Safari yao itaanza kwa mchezo mgumu dhidi ya Mafunzo utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, ambao unatarajiwa kuwa mtihani wa kwanza kwa Wekundu wa Msimbazi.

Simba wanaingia katika mashindano hayo wakiwa na morali kubwa na matumaini ya kufanya vizuri, wakilenga kuanza kwa ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele na kuendeleza kasi yao ya ushindani katika michuano hiyo.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo ina malengo mawili makubwa, kushinda mechi zote na hatimaye kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano, kila mchezo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kikosi.

Ahmed ameongeza kuwa kikosi kilichosafiri kina wachezaji wote muhimu isipokuwa wale wenye majeraha, amebainisha kuwa michuano hiyo ni zaidi ya kutafuta kombe, bali pia ni fursa ya kuimarisha kikosi kuelekea mechi zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba wameweka wazi kuwa michuano hiyo itawasaidia kuongeza ubora wa timu kabla ya Kariakoo Derby, mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali na mvuto mkubwa kwa mashabiki.

Ikiwa Simba na Yanga zote zitafika hatua ya fainali, basi huenda zikakutana tena Zanzibar kabla ya kuhamishia upinzani wao katika Derby ya Mei 3, 2026.