HABARI njema zimeanza kutanda ndani ya kikosi cha Simba SC kufuatia mshambuliaji wao hatari, Mohammed Bajeber, kurejea kwenye ushindani baada ya kuuguza majeraha kwa muda.
Nyota huyo sasa amepewa ruhusa ya madaktari kurejea uwanjani, hatua inayoongeza nguvu mpya ndani ya kikosi hicho.
Bajeber ni sehemu ya wachezaji waliosafiri na Simba chini ya Kocha Steven Barker kuelekea Visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Muungano. Uwepo wake unapanua wigo wa chaguo katika safu ya ushambuliaji, hasa wakati timu ikijiandaa kwa mechi muhimu dhidi ya Mafunzo SC.
Katika maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo, mshambuliaji huyo alionekana kuwa katika hali nzuri kimwili na kiuchezaji. Alishiriki mazoezi kikamilifu, akionyesha ari, nguvu na hamu ya kurudi uwanjani kwa kasi baada ya kipindi kirefu cha kukaa nje.
Uwepo wa Bajeber kambini umeleta msukumo chanya kwa wachezaji wenzake, huku morali ya timu ikiongezeka kwa kiasi kikubwa. Wachezaji wanaonekana kuwa na imani zaidi, wakijua wana silaha nyingine muhimu kwenye safu ya ushambuliaji.
Kocha Steven Barker anatarajiwa kutumia michuano hii kama fursa ya kuwarejesha taratibu nyota wake waliokuwa majeruhi. Mkakati wake ni kuwapa dakika za kutosha ili warejee kwenye kiwango chao bora, huku akihakikisha timu inabaki kuwa na ushindani mkubwa.
Pamoja na hilo, Simba inaingia kwenye michuano ya Kombe la Muungano ikiwa na malengo makubwa ya kutwaa ubingwa. Kocha Barker anataka kuongeza kombe jingine kwenye kabati la mafanikio ya klabu hiyo, jambo linaloifanya timu kupambana kwa ari ya hali ya juu.
Kurejea kwa Bajeber, Simba imepata nguvu mpya muhimu, uwezo wake wa kufumania nyavu na kasi yake uwanjani vinatarajiwa kuwa tishio kwa wapinzani, mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona kama ataanza kung’ara mara moja dhidi ya Mafunzo SC