Albert Kangwanda Yanga
Yanga SC

Kangwanda Afichua Siri ya Bao la Ushindi Dhidi ya Simba Ngao ya Jamii

Vardo August 13, 2026 8:18 am

DAR ES SALAAM: Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga SC, Albert Kangwanda, ameweka wazi siri iliyomfanya afunge bao la ushindi lililowapa ubingwa wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC.

Mzaliwa huyo wa Luanshya nchini Zambia, alipachika goli hilo pekee la ushindi kwa kichwa katika dakika ya 31 ya mchezo, akimalizia krosi safi iliyopigwa kutoka upande wa kushoto na Chadrack Boka na kumwacha kipa Mahamadou Kassali asijue la kufanya.

Ushindi huo wa 1-0 uliopatikana leo Jumatano, Agosti 12, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar, umeifanya Yanga kutwaa taji la Ngao ya Jamii kwa mara ya tatu mfululizo.

Akizungumza na Azam TV mara baada ya mchezo huo kumalizika, Kangwanda alisema alitambua mapema kuwa dabi hiyo ingekuwa ngumu, lakini kufunga goli mbele ya mashabiki wengi kumempa morali kubwa kuelekea msimu mpya.

“Kabla ya mchezo nilijua hautakuwa rahisi. Kufunga katika mchezo mkubwa wa dabi mbele ya mashabiki wenye hamasa kubwa ni jambo linalonipa moyo na kunitia nguvu zaidi. Sasa akili yangu yote ipo kwenye mechi zijazo,” alisema Kangwanda.

Mzambia huyo aliongeza kuwa goli hilo limeongeza kujiamini kwake katika maisha yake mapya ndani ya Wananchi, huku akisisitiza kuwa furaha yake kubwa ni kuona timu inapata matokeo chanya.

Mbinu za Kocha Zazaa Matunda

Kangwanda alibainisha kuwa goli hilo halikuwa la bahati mbaya, bali ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo ya kocha wake, Manqoba Mngqithi, kuhusu namna mawinga wanavyopaswa kuingia eneo la hatari.

“Kocha amekuwa akitisisitiza mawinga kushambulia lango muda wote. Kila mpira unapokuwa upande wa pembeni, unatakiwa kukimbilia langoni kutafuta nafasi. Boka alipopiga krosi, mpira ulinikuta mahali sahihi na kazi yangu ilikuwa ni kuuelekeza golini. Pongezi nyingi ziende kwa Boka kwa krosi ile safi,” aliongeza Kangwanda.

Kangwanda alijiunga na Yanga katika dirisha hili kubwa la usajili akitokea klabu ya Red Arrows ya Zambia, na bao hili linatajwa kuwa mwanzo mzuri wa safari yake ndani ya klabu hiyo kuelekea msimu wa 2026-2027.

Albert Kangwanda Ailaza Simba, Yanga Kutwaa Ngao ya Jamii 2026/27 New Amaan Said Mussa Mbeki Ajiunga na KVZ: Sababu za Kuondoka Mlandege na Mipango Mipya