WAKATI mbio za ubingwa wa Kombe la Muungano zikizidi kupamba moto zikihusisha Yanga, Azam FC, Singida BS pamoja na Simba SC, Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Steve Barker, ameweka wazi mkakati wake maalum unaolenga kuipa timu yake makali ya ziada.
Barker amesema analiangalia Kombe la Muungano kama zaidi ya mashindano ya kawaida, akieleza kuwa ni jukwaa muhimu la kujenga kikosi imara chenye ushindani mkubwa na utayari wa kukabiliana na changamoto za ndani na kimataifa.
Akizungumzia malengo yake, Barker ameweka wazi kuwa kipaumbele cha kwanza ni kutwaa ubingwa wa michuano hiyo. Anaamini kila taji lina mchango mkubwa katika historia ya klabu na kuongeza hali ya kujiamini kwa wachezaji wake.
“Ushindi kwenye Kombe la Muungano utakuwa kichocheo muhimu kwa Simba SC kuelekea majukumu mengine ya ndani na nje ya nchi,” alisema Barker, akisisitiza dhamira ya kuona timu yake inatwaa kombe hilo.
Mbali na hilo, kocha huyo ameeleza kuwa anatumia mashindano hayo kuwapa nafasi wachezaji ambao hawapati muda wa kutosha katika mechi kubwa. Lengo ni kupima uwezo wao, kuwajengea uzoefu na kuongeza ushindani wa ndani ya kikosi.
Sambamba na hilo, Barker amesisitiza umuhimu wa kuijenga upya timu kiakili. Baada ya kupitia vipindi vigumu vya ligi, anataka kuona wachezaji wake wakirejea wakiwa na ari mpya, mshikamano imara na njaa ya ushindi.
Barker anaona Kombe la Muungano kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha msingi wa timu, akiamini kuwa mafanikio katika malengo hayo matatu yataifanya Simba SC kurejea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na nguvu mpya na kuwa tishio kubwa zaidi kwa wapinzani wao.