KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite Queens), Bakari Shime, ametaja kikosi cha wachezaji 27 kitakachoingia kambini kujiandaa na michezo miwili ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Cameroon.
Akizungumza wakati wa kutangaza kikosi hicho, Shime amesema wachezaji aliowachagua wanafahamu uzito wa jukumu lililopo mbele yao, akisisitiza kuwa ni nafasi muhimu kwa Tanzania kuandika historia ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
“Wachezaji tuliowaita wanaelewa umuhimu wa hatua hii. Ni michezo muhimu kwa taifa, na jukumu limekuwa kubwa zaidi kwa sababu Tanzania inalenga kufuzu fainali za Kombe la Dunia,” amesema Shime.
Ameongeza kuwa benchi la ufundi limejipanga kuhakikisha linawaandaa vyema wachezaji hao ili waweze kufanya vizuri katika michezo hiyo miwili.
“Tuna michezo miwili, wa kwanza utachezwa Cameroon, hivyo tunapaswa kupata matokeo mazuri ugenini kisha kumalizia nyumbani mbele ya Watanzania,” amesisitiza.
Shime amebainisha kuwa maandalizi ya kikosi hicho yatalenga kuimarisha mbinu na morali ya wachezaji ili waweze kukabiliana na ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao.
Wachezaji walioteuliwa ni Nusrat Jaffar, Asha Omary, Diana Mnally, Winfrida Castro, Ester Maseke, Lidya Maximilian, Hasnat Ubamba, Aliya Fikiri, Jamila Rajab, Yasinta Mitoga, Winfrida Gerald na Zulfa Makau.
Wengine ni Zawadi Hamis, Mary Siyame, Elizabeth Joseph, Neema Paul, Bahati Steven, Harrier Juma, Yasinta Michael, Rhobi Daudi, Sarah Joel, Fatuma Hamis, Neema Mtunzi, Zuhura Mlekwa, Veronica Mapunda, Hellen Hamis pamoja na Christer Basil.