MANCHESTER City inafikiria kufanya jaribio la kumsajili kiungo wa Chelsea na timu ya taifa ya Argentina, Enzo Fernández, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Fernandez ni mmoja wa viungo bora wa kizazi chake na mara kadhaa msimu huu amekuwa akihusishwa na Real Madrid ambayo amewahi kutamka hadharani watoto wake wangependelea kuishi katika mji huo.
Hali hiyo ilisababisha asimamishwe kucheza mechi mbili ikiwa ni sehemu ya adhabu aliyopewa na benchi la ufundi.
Manchester City inataka kuboresha eneo lao la kiungo msimu ujao kwani baadhi ya mastaa wao muhimu ikiwamo Benardo Silva wanatarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu.
Licha ya vigogo wengi kuonyesha nia ya kumsajili staa huyu ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2032, Chelsea haionekani kuwa tayari kumwachia kirahisi.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka vyanzo vya ndani ya Chelsea, Enzo mwenyewe ameshawasilisha maombi ya kutaka kuondoka ili kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.
Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 48 za michuano yote na kufunga mabao 12.
James Trafford
ASTON Villa imeonyesha nia ya kumsajili kipa wa Manchester City na England, James Trafford, 23, dirisha lijalo.
Villa inamtazama Trafford kama mbadala wa muda mrefu wa kipa wao wa kimataifa wa Argentina, Emiliano Martinez, 33, ambaye umri umeshaanza kumtupa mkono.
Kwa mujibu wa ripoti, Trafford mwenyewe amekuwa akitamani sana kuondoka mwisho wa msimu huu ili kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa ya kucheza tofauti na ilivyo sasa.
Rafael Leao
KLABU kubwa Ulaya zimeanza kumfuatilia kwa karibu winga wa kimataifa wa Ureno, Rafael Leao, 26, anayekipiga AC Milan.
Miongoni mwa klabu kubwa zinazomhitaji ni pamoja na Liverpool, Manchester United, Manchester City pamoja na Real Madrid.
Mabosi wa Milan wapo tayari kumuuza Leao lakini wanahitaji ofa isiyopungua Pauni 60 milioni. Kwa sasa mazungumzo baina ya wawakilishi wa timu tajwa hapo juu na Milan yamekuwa yakiendelea.
Carlos Baleba
MANCHESTER United imewaweka katika rada mastaa wawili kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Wachezaji hao ni pamoja na beki wa Tottenham Hotspur na Uholanzi, Micky van de Ven, 25, pamoja na kiungo wa Brighton na timu ya taifa ya Cameroon, Carlos Baleba, 22, ambaye ana uwezo mkubwa wa matumizi ya nguvu.
Mastaa hao kwa jumla wanaweza kuigharimu Man United zaidi ya Pauni 100 milioni kama ada ya uhamisho.
Elliot Anderson
MANCHESTER City inaongoza katika vita ya kumsajili kiungo wa Nottingham Forest England, Elliot Anderson, 23, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Licha ya ushindani kutoka kwa Manchester United na Arsenal.
Man City wanaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi kwa sasa ya kufanikisha dili hilo na inadaiwa imeshafikia hadi makubaliano binafsi na wawakilishi wake. Anderson ana uwezo mkubwa wa kucheza kama kiungo wa kati.
Jadon Sancho
WINGA wa Manchester United ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Aston Villa, Jadon Sancho, ameripotiwa kuwaambia mabosi wa Borussia Dortmund yupo tayari kujiunga nao dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mazungumzo kati ya pande mbili tayari yanaendelea, yakilenga kufanikisha dili hilo ambalo linaweza kumrudisha Sancho kwenye klabu aliyowahi kung’ara nayo kabla ya kuhamia Manchester United.
Dortmund inaamini kurejea kwa Sancho kunaweza kuongeza nguvu katika safu yao ya ushambuliaji kwani anaifahamu vizuri timu.
Yan Diomande
WAKALA wa winga wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yan Diomande, 19, tayari amefanya mazungumzo na Liverpool na Paris Saint-Germain kuhusu uwezekano wa kujiunga na moja kati ya klabu hizo.
Hata hivyo, RB Leipzig ina msimamo wa kutaka kumbakisha nyota huyo kwa angalau msimu mmoja zaidi ili aendelee kukua na kupata uzoefu ndani ya kikosi.
Vilevile Leipzig inataka staa huyo acheze kwa msimu mmoja zaidi ili thamani yake ipande zaidi.






