Taarifa za kitabibu zinaeleza jeraha hilo linaweza kumweka nje kwa muda wote uliosalia wa msimu, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa Barcelona ambao wanaongoza LaLiga kwa alama 82.
Kukosekana kwake kunamaanisha kupungua kwa ubunifu, kasi na hatari katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona, ambayo imekuwa ikimtegemea katika mechi muhimu za msimu huu.
Kwa upande wa Real Madrid, hatari iko kwa Mbappé ambaye ana kadi nne za njano katika LaLiga. Akipata kadi moja zaidi atafungiwa na hivyo kuikosa El Clasico.
Mshambuliaji huyo Mfaransa, ambaye amefunga mabao 24 katika mechi 27 za ligi msimu huu, amekuwa nguzo muhimu kwa Real Madrid katika mbio za ubingwa, lakini nidhamu yake uwanjani imeanza kumweka kwenye hatari kubwa ya kufungiwa.
Barcelona inaongoza ligi kwa alama 82 dhidi ya 73 za Real Madrid, hivyo El Clasico hii ina uzito mkubwa katika kuamua bingwa wa msimu.
Kukosekana kwa Yamal na Mbappé kunaweza kupunguza ubora na mvuto wa dabi hiyo, pia kunaweza kuwapa nafasi wachezaji wengine kujitokeza katika mechi yenye presha kubwa na macho ya dunia yote.