Home Habari za michezo GAMONDI AITAKA ZANZIBAR KUPANDISHA UBORA WA LIGI YAKE

GAMONDI AITAKA ZANZIBAR KUPANDISHA UBORA WA LIGI YAKE

0

LIGI ya Zanzibar imeelezwa kumpa wakati mgumu kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Miguel Gamondi, kutokana na kutokuwepo kwa ushindani mkubwa kama ilivyo kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Gamondi amebainisha kuwa tofauti ya ubora kati ya timu za Zanzibar na zile za Bara imeonekana wazi, hususan baada ya kufuatilia mashindano ya Kombe la Muungano yaliyozikutanisha timu kutoka pande zote mbili.

Amesema katika uchunguzi wake, amegundua kuwa kiwango cha ushindani kwenye Ligi ya Zanzibar bado kiko chini, jambo ambalo linafanya baadhi ya timu kubwa kutoka Bara kupata ushindi kirahisi hata zinapofanya mabadiliko ya vikosi vyao.

“Timu za Zanzibar zipo chini kiushindani japo iliyopelekea Yanga na Azam FC kushinda kirahisi licha ya kufanya mabadiliko ya vikosi vyao,” amesema Gamondi akifafanua hali hiyo.

Ameongeza kuwa hali hiyo ni changamoto kwa maendeleo ya soka la taifa, kwani ligi zenye ushindani mdogo zinaweza kuathiri ubora wa wachezaji wanaoingia kwenye timu ya Taifa.

Gamondi amesisitiza kuwa kuna haja ya dharura ya kupandisha kiwango cha Ligi ya Zanzibar, akibainisha kuwa tayari amekutana na baadhi ya makocha wa visiwani humo kwa ajili ya kutoa muongozo wa namna ya kuinua vipaji na kuongeza ushindani.