Home Habari za michezo HAKUNA UNYONGE, NI UBORA TU, SIMBA YAWINDA YANGA FAINALI

HAKUNA UNYONGE, NI UBORA TU, SIMBA YAWINDA YANGA FAINALI

0

MACHO na masikio ya wadau wa soka nchini kwa sasa yameelekezwa visiwani Zanzibar, wakisubiri kwa hamu kuona kama ndoto ya fainali ya Kombe la Muungano kati ya Simba na Yanga itatimia. Hii ni kutokana na ubora na ushindani mkubwa wa vikosi vya timu hizo mbili kongwe.

Simba tayari imetinga hatua ya nusu fainali, ambapo itashuka dimbani kesho kuivaa Mlandege SC. Mshindi wa mchezo huo atafuzu kucheza fainali dhidi ya atakayeshinda nusu fainali ya pili kati ya Yanga SC na Azam FC.

Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea kesho katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, huku kila timu ikiwa na lengo moja tu, ushindi wa kutinga fainali na kuwania ubingwa.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi msimamo wa klabu hiyo kuwa wanaitamani kukutana na watani wao wa jadi, Yanga SC, katika fainali.

Amesema ndani ya kikosi cha Simba kuna ari kubwa na hamasa ya hali ya juu, huku wachezaji pamoja na benchi la ufundi wakiwa tayari kupambana kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanavuka salama hatua ya nusu fainali.

Ahmed amesisitiza kuwa Simba haina hofu na mpinzani yeyote, akibainisha kuwa lengo lao kuu ni kufika fainali na kukutana na Yanga, ili kuthibitisha ubora wao kwenye jukwaa kubwa la michuano hiyo.

“Sisi Simba tupo Zanzibar hadi mwisho wa mashindano. Hatufikirii kuishia nusu fainali, na suala la Mlandege SC tutakabiliana nao ipasavyo,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa nguvu zote kwa sasa zimeelekezwa kwenye mchezo dhidi ya Mlandege SC, akisisitiza kuwa ushindi ni jambo lisiloweza kuepukika kwani ndiyo tiketi pekee ya kufungua mlango kuelekea fainali wanayoitamani.

“Sisi tunamhitaji Yanga, hakuna kukimbia mtu. Wao wakacheze nusu fainali yao, na sisi tunaenda kupambana na Mlandege SC kuhakikisha tunashinda ili tukutane nao fainali,” ameongeza.

Kauli hiyo imezidi kuongeza presha na hamasa kwa mashabiki wa soka nchini, hasa ukizingatia ukubwa wa dabi ya Kariakoo kati ya Simba SC na Yanga SC, ambayo mara nyingi huleta ushindani mkali na burudani ya kipekee.